Katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Kijiji cha Rubao, Kata ya Ijumbi Wilayani Muleba Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Dkt Abel Nyamahanga amewahimiza wazazi kuhakikisha wanawalinda watoto kutojihusisha na mitandao ya kijamii ambayo inaweza kuharibu mienendo, tabia na maadili yao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya amewaeleza wazazi kuwa kupitia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema "Zingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa kidigitali" ni vyema wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha kwamba usalama wa watoto unazingatiwa na kuwawekea mazingira salama yanayowazunguka hasa wanapokuwa wakiitumia mitandao ya kijamii.
"Sisi wazazi ni lazima tuwakinge watoto wetu wasijiingize kwenye mitandao hii ambayo inaweza ikaharibu tabia yao na mwenendo wao kwa namna ambavyo watakuwa wakiitumia mitandao hiyo" amesema Mhe. Dkt Abel Nyamahanga.
Aidha, amewahimiza wananchi kuacha matendo ya kiukatili hasa matendo ya mauaji ambayo yanasababisha watoto kubakia wakiwa yatima jambo ambalo linapelekea watoto hao kutendewa vitendo ambavyo si rafiki kwa sababu ya kukosa wazazi wao.
Lakini pia amewahimiza wazazi kuwaruhusu watoto kushiriki katika mabaraza pamoja na michezo mbalimbali wawapo mashuleni jambo ambalo litawasaidia kuwajengea uwezo wa kujiamini na kujieleza.
Sambamba na hayo amewahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia, Polisi, Walimu na Wadau wengine wote kuendelea kutoa huduma ya elimu ya malezi na makuzi ya watoto kwa wazazi na walezi ili waelewe wajibu wao wa kulea watoto katika msingi wa haki na usawa wa kijinsia.
Katika risala iliyosomwa na Adiria Adronikus mmoja wa watoto walioshiriki maadhimisho hayo amesema kuwa kwa kipindi cha kuanzia july 2022 hadi april mwaka huu jumla ya vitendo vya kikatili 1,344 vimefanyika kwa watoto katika Wilaya ya Muleba ikiwemo ukatili wa kimwili, kihisia na wa kingono huku jumla ya wanafunzi 11 wakibainika kuwa na ujauzito wanafunzi 7 wakiwa wa shule ya Sekondari na wanafunzi 4 wakiwa wa shule ya msingi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa