Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe.Hajjat Fatma Mwassa amekabidhi Mwenge wa uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.Martin Shigella ukitokea Mkoa wa Kagera katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba tarehe 30/09/2024.
Makabidhiano hayo yamefanyika mbele ya Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Ndugu, Godfrey Eliakimu Mzava katika eneo la uwanja wa Shule ya Sekondari Bwongera iliyopo katika Kijiji cha Kitete Kata ya Bwongela Wilaya ya Chato Mkoani Geita.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 Mkoani Kagera zimehitimishwa ambapo tarehe 22 Septemba Mwenge wa uhuru uliingia Mkoani Kagera ukitokea Mkoa wa Kigoma na hivyo kumaliza mbio zake tarehe 29/09/2024 katika Wilaya ya Muleba kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Geita.
Mwenge wa uhuru ukiwa Kagera, umekimbizwa katika Halmashauri nane ambazo ni Halmashauri ya Biharamulo, Ngara, Karagwe, Kyerwa, Missenyi, Bukoba, Muleba na Manispaa ya Bukoba kwa umbali wa kilomita 1,165.
Mwenge wa Uhuru ulitembelea jumla ya Miradi 55 yenye thamani ya shilingi bilioni 54.7 na kati ya hiyo,miradi 14 iliwekewa mawe ya msingi,miradi 5 ilifunguliwa,miradi 18 ilizinduliwa na miradi 18 ilitembelewa na kuonwa na Mwenge wa Uhuru, ikiwa ni pamoja na kutoa misaada kwa shule zenye watoto wenye mahitaji maalum na hivyo kufanya Miradi yote 55 kukubaliwa.
Aidha,Kiongozi wa Mbio za mwenge wa uhuru ndugu Godfrey Mzava ameupongeza mkoa wa Kagera kwa kazi kubwa iliyofanyika katika usimamizi wa miradi pamoja na kuupokea Mwenge wa Uhuru kwa shamra shamra na hamasa kubwa ulipopita katika maeneo yote ya Mkoa wa Kagera.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa