Katika Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika ndani ya Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dkt Abel Nyamahanga ametoa onyo kwa wanaohujumu miradi ya maendeleo kuacha vitendo hivyo kabla ya hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Akizungumza Katika Baraza hilo Mkuu wa Wilaya amewasihi Watumishi pamoja Watendaji kuhakikisha wanatekeleza miradi kwa viwango bora vinavyostahili.
"Kama darasa lilitakiwa lijengwe kwa mita saba ikaongezeka ikawa mita saba na nusu au madarasa matano yakaongezewa kwa utaratibu huo tafsiri yake kama fedha haijaongezwa maana yake mradi huo upo chini ya kiwango na kama ni darasa likafinywa labda ilikuwa inatakiwa iwe mita saba ikajengwa mita sita tafsiri yake ni kwamba mradi huo umehujumiwa" amesema Mhe. Dkt Abel Nyamahanga.
Aidha, amesema kuwa lipo tatizo la kujenga miradi kwenye maeneo ambayo yana migogoro hivyo ameshauri kuepuka utaratibu wa kujenga miradi kwenye maeneo yenye migogoro badala yake yatafutwe maeneo ambayo hayana migogoro ndipo miradi ijengwe.
Sambamba na hayo amesema kuwa baadhi ya Viongozi wakiwemo Wenyeviti wamekuwa vyanzo vya migogoro kwa wananchi hivyo amewasihi kuhakikisha wanakuwa wasuruhishi wa migogoro na sio kuwa sehemu ya migogoro hiyo.
Lakini pia amewaagiza Maafisa Ugani kuwatembelea wananchi kuwapa elimu bora ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kusafisha mashamba yao na kutunza mashamba yao pamoja na kuhakikisha wanashirikiana na Watendaji, Madiwani na Wenyeviti wa vijiji kuhakikisha kila Kijiji kinakuwa na Shamba darasa ambalo litaleta tija katika kilimo bora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus amewasihi Madiwani, Watendaji pamoja na Wakuu wa Sehemu na Vitengo kuongeza umakini katika utendaji kazi wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na usimamizi bora wa miradi ili iweze kutekelezeka kwa viwango vinavyostahili.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Evart Kagaruki katika utekelezaji wa miradi amewasihi Madiwani kuishirikisha Ofisi ya Mkurugenzi ili unapoanza utekelezaji wa miradi hiyo mhandisi awepo eneo husika kuona hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa mradi kwa lengo la kuhakikisha ubora unazingatiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa