Katika maadhimisho ya Siku ya Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa Duniani yaliyofanyika Kiwilaya katika Kata ya Muleba eneo la Uwanja wa Zimbihile na Uwanja wa Fatuma, wananchi wameendelea kuhimizwa kuchanja mbwa wao mara kwa mara kila baada ya mwaka ili kuwaepushia tatizo la kupata ugonjwa wa Kichaa cha mbwa.
Akizungumza kabla ya kutoa chanjo kwa baadhi ya Mbwa walioletwa na wananchi ili waweze kupatiwa chanjo hiyo wakiwa na uelewa wake, Bi. Joyce Kombe Daktari wa mifugo Wilayani Muleba, amewaelezea wananchi kuwa Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa ni ugonjwa hatari sana ambao unaweza kuambukizwa kwa mbwa na huyo mbwa akamuambukiza binadamu kwa kumng'ata jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya binadamu.
"Unaweza kumtambua mbwa mwenye dalili ya Kichaa pale ambapo utamuona mbwa wako alikuwa amezoea kuchangamka mara ghafla ukaona ameacha kuwa na hali hiyo au akawa mkali sana, akaanza kuwa na dalili za kung'ata vitu au ukamuona anaanza kutiririsha mate kutoka mdomoni, hizo ni baadhi ya dalili za mbwa mwenye virusi vya Kichaa cha mbwa" amesema Daktari Kombe.
Naye Ndg. Geofrey Kisai ambaye ni Afisa Mifugo Kata ya Izigo ameongeza kwa kuwaeleza wananchi kuwa kama mwananchi mmoja akichanja mbwa wake lakini jirani yake akawa na yeye ana mbwa ila hajachanjwa kuna uwezekano mkubwa wa mbwa huyo ambaye hajachanjwa akamuambukiza mbwa ambaye amechanjwa hivyo amewahimiza wananchi wote kuwa ni vema wakawa na desturi ya kuchanja mbwa wao mara kwa mara kila zoezi la chanjo linapofanyika.
Kwa upande wake Siperatus Angelo mkazi wa Kata ya Muleba ameshauri kuwa ni vema wananchi wakawa wanawapeleka mbwa wao kupatiwa chanjo hata kwenye vituo vya afya ili kuweza kuwaepusha mbwa wao kupata maradhi ya kichaa cha mbwa.
Datius Kalinjuma Salvatory mkazi wa Kata ya Muleba ameeleza kuwa mbwa akichanjwa inasaidia kuishi kwa amani pamoja na wananchi wengine kwani mbwa akipata ukichaa kama hajachanjwa anaweza kumjeruhi mwanadamu na kumuambukiza ugonjwa wa ukichaa jambo ambalo linaweza kuleta athari katika jamii.
Katika maadhimisho hayo jumla ya mbwa 304 na paka 27 wamepatiwa chanjo ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa