Katika zoezi la kukabidhi vishikwambi Kwa walimu wa Shule za Sekondari na Shule za Msingi lililofanyika katika shule ya Sekondari Kaigara Wilayani Muleba Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus amewahimiza walimu kuvitunza vishikwambi hivyo na kuvitumia kwa matumizi sahihi yanayohusiana na Taaluma.
Akizungumza baada ya kukabidhi vishikwambi hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba amesema kuwa mwalimu anaruhusiwa kutumia picha za video vitini vya masomo alivyovichukua kutoka taasisi ya elimu ya Tanzania katika kishikwambi hicho kufundishia na kurahisisha utendaji wa kazi zao.
"Ni vema mkahakikisha mnavitunza vizuri vishikwambi hivi na sio lazima uende nacho kila mahali lakini wakati wa kazi unaweza ukakichukua ukakitumia katika kutekeleza majukumu yako" amesema Mhe. Magongo Justus.
Lakini pia amewasisitiza walimu kuhakikisha wanasimamia taaaluma kwa bidii ili kuweza kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora na inayostahili ili kuweza kusaidia wanafunzi kuwa na ufaulu mzuri katika mitihani yao.
"Tunahitaji Mkuu wa matokeo sio Mkuu wa shule wa kukalia kiti tu na ndio maana nimesisitiza tunahitaji msimamie taaluma kwa kiwango kinachostahili ili wanafunzi waweze kupata elimu bora" ameongeza Mhe. Magongo Justus
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Elias Kayandabila amewasihi walimu kuvitunza vishikwambi katika mazingira salama ili visiweze kuibiwa kwa kusudi la kuweza kusaidia katika utunzaji wa kumbukumbu na kurahisisha utendaji wa kazi zao.
Katika risala iliyosomwa na Afisa Elimu Sekondari Ndg. Jared Muhile amesema kuwa Halmashauri imepokea jumla ya vishikwambi 2204 na kuelekeza vigawiwe Kwa Maafisa Elimu Ngazi zote za Halmashauri kata na walimu wote wa katika shule za msingi na Sekondari.
Aidha, amesema kuwa endapo Mwalimu atakoma utumishi wa umma kwenye kada ya ualimu aidha kusitaafu kuacha kazi au kufariki au kuhama kada ya ualimu atalazimika kukabidhi kishikwambi hicho kwa mkuu wa kituo chake cha kazi na vishikwambi hivyo vitatumika kwa matumizi ya kujifunzia na kufundishia kwa walimu wa shule za msingi na Sekondari.
Mwalimu Charles Mkaluka kaimu Mkuu wa Shule ya Kiteme Sekondari amesema kuwa vishikwambi hivyo vitaweza kuwasaidia kuwarahisishia walimu kazi ya kupeluzi maswali na kupata mambo mengine mengi kama video na picha mbalimbali ambazo zinaweza kutumika katika kufundishia wanafunzi.
Naye Melines Maluka Afisa elimu kata wa Mayondwe ameeleza kuwa zoezi la ugawaji wa vishikwambi kwa walimu litazaa matunda makubwa naazuri katika uendeshaji wa zoezi la ufundishaji wa wanafunzi katika shule za Sekondari na shule za Msingi.
Anord Rweyemamu Byabato Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ruhanga ameeleza kuwa vishikwambi hivyo vitawarahisishia kazi ya utunzaji wa takwimu ambapo amesema kuwa hapo awali walikuwa wakitumia mafaili kutunza nyaraka na wakati mwingine nyaraka zilikuwa zinapotea lakini kwa kutumia vishikwambi hivyo vitaweza kuwarahisishia kazi hiyo.
Jumla ya Vishikwambi 2204 vimegawiwa kwa walimu ambapo Idara ya elimu Sekondari wamepokea jumla ya vishikwambi 764 na shule za msingi wamepokea jumla ya vishikwambi 1398 na maafisa elimu kata wamepokea jumla ya vishikwambi 42.
Imetolewa na:
kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa