Katika kikao kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dkt Abel Nyamahanga amewahimiza viongozi kuendelea kutoa ushirikiano wa pamoja na kulifanya zoezi la kupambana na uvuvi haramu kuwa endelevu ili kuweza kukomesha uvuvi haramu wilayani Muleba.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya amewahimiza Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji, Maafisa Uvuvi, Wenyeviti wa BMU, Wenyekiti wa Vijiji na Vitongoji kuhakikisha wanatenda kazi ya kupambana na uvuvi haramu kwa haki na kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vya Rushwa ambavyo vinaweza kupelekea vitendo vya uvuvi haramu kuendelea kuwepo.
"Heshima ya kiongozi inakuja kutokana na namna unavyosimamia haki, tutende haki ibaki kutenda haki afadhari uhukumiwe usulubiwe kwa kutenda haki kuliko kusulubiwa kwa kutenda kwa ubadhirifu" amesema Mhe. Dkt Abel Nyamahanga.
Aidha ametoa onyo kwa viongozi ambao wanashiriki katika vitendo vya uvuvi haramu kuacha tabia hiyo kabla ya hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Lakini pia amewaomba na kuwasihi wananchi wanaoshiriki katika vitendo vya uvuvi haramu kufanya shughuli zilizo harali na sio kwenye uvuvi haramu ili kuweza kulinda na kukuza mapato ya Halmashauri ambayo kwa asilimia 53 yanatokana na uvuvi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Jared Muhile akizungumzia pendekezo la kurudisha asilimia 5 za mapato yanayopatikana kutokana na uvuvi ili iweze kutumika katika zoezi la kupambana na uvuvi haramu amesema kuwa watakaa na Mkuu wa Kitengo cha Uvuvi ili kuliweka kwenye mpango wa bajeti kwa lengo la kuhakikisha wanaondoa changamoto hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Bugasha Kata ya Mayondwe Ndg. Nathani Matungwa ameshauri kufungwa kwa mialo bubu ambayo haijasajiliwa inayotumiwa na wavuvi haramu jambo ambalo litasaidia kupunguza kasi ya uvuvi haramu.
Naye Mtendaji wa Kata ya Bumbire Marrygoreth Gelvazi amesema kuwa uvuvi haramu wa kutumia makokoro unahatarisha uwepo wa samaki ziwani na kuharibu mazalia ya samaki hivyo ameshauri kuendelea kufanyika zoezi la kupambana na uvuvi haramu ili kuweza kukomesha matumizi ya nyavu haramu.
Katika kikao cha kujadiri na kupanga mikakati ya kupambana na uvuvi haramu kilichofanyika tarehe 17/04/2023 na kuadhimia wavuvi wanaotumia nyavu haramu kurejesha nyavu haramu ndani ya siku saba, zaidi ya dhana haramu 1229 zimerejeshwa zikiwemo timba 977, makila 85, makokoro 155 pamoja na mitumbwi 8.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa