Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dkt. Abel Nyamahanga amewataka Viongozi wa Umma kuviishi viapo walivyo apa hasa kiapo cha ahadi ya uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao na pia kuepukana na vitendo vya migongano ya maslahi ili kujenga imani kwa wananchi wanaowaongoza.
Mhe.Dkt. Abel Nyamahanga ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua Mafunzo ya Viongozi kuhusu Maadili yaliyoendeshwa na Maafisa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba tarehe 23 Januari 2024.
Akizungumza katika hotuba yake Dkt.Abel amesema kuwa “Serikali inatoa fedha nyingi za Miradi katika Halmashauri nyingi Nchini na hivyo ili Miradi ikamilike kwa ubora na kwa wakati lazima rasilimali hizo zipate usimamizi mzuri wa Viongozi”
Aidha, Mhe.Dkt.Abel Nyamahanga ameongeza kuwa Viongozi wa Umma wanayo dhamana kubwa katika kusimamia Rasilimali za Umma kwa umakini na Uadilifu mkubwa ili kujenga imani kwa Wanannchi wanaowaongoza,pia Dkt.Nyamahanga amewataka viongozi kuzingatia maelekezo ya Serikali katika utendaji kazi kwa kufanya maamuzi sahihi kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Awali akieleza lengo la mafunzo hayo katibu msaidizi Sekretarieti ya maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Godson Kweka aliwakumbusha Viongozi kujiepusha na vitendo vyote vinavyopelekea uwepo wa migogoro wa Maslahi na kuwataka Viongozi hao kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ili kujenga imani kwa wananchi wanaowaongoza.
Bw. Kweka pia amewataka Viongozi kusimamia Rasilimali za Umma kwa uadilifu mkubwa hasa pesa za miradi mbalimbali ya Halmashauri na kuhusu urejeshaji wa tamko la Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma kwa mwaka jana 2023 ambapo amefafanua kuwa asilimia 90% ya Viongozi wote wa Halmashauri ya Muleba walirejesha matamko yao kwa wakati.
Aidha mafunzo hayo ya Maadili ya Viongozi wa Umma yamehudhuriwa na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba zaidi ya 100 kutoka katika Idara, Vitengo pamoja na waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Imeandaliwa na kutolewa na;
Eusebius J. Kiluwa
KAIMU MKUU KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa