Halmashauri ya wilaya ya Muleba ni miongoni mwa Halmashauri 186 zinazotekeleza sheria ya kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya kina mama, vijana na watu wenye walemavu. Kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri imekuwa ikitoa elimu na hamasa kwa jamii ili kujiunga katika vikundi, kuanzisha na kuwa na biashara na kisha kuwapa mikopo inayowawezesha kukuza mitaji yao lakini pia kujikimu kimaisha.
Vikundi hivi hujishughulisha na kilimo, uvuvi, ufugaji pamoja na biashara ndogo ndogo. Kutokana na mikopo hiyo walengwa wameweza kunufaika kwa kuongeza mitaji katika biashara zao na kupitia kukua kwa biashara zao wameweza kumudu kuwalipia watoto ada za shule, kuwanunuliwa wanafunzi sare za shule na kumudu gharama za matumizi ya kawaida katika familia na maisha ya kila siku.
Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2020, Halmashauri iliwezesha vikundi hivyo jumla ya Tshs. 1,716,363,642.00 ikiwa ni 10% ya Mapato yake ya ndani pamoja na fedha za marejesho, kwa ajili ya utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa makundi maalumu. Mikopo hiyo ilitolewa kwa vikundi 625, kwa mchanganuo ufuatao ambapo vikundi vya wanawake (WDF) vilikuwa vikundi 465 vilikopeshwa jumla ya Tsh. 986,753,306.00, vikundi vya Vijana (YDF) 139 vilikopeshwa Tsh. 683,076,973.00 na vikundi vya watu Watu wenye ulemavu (DISABLED) 21 vilikopeshwa kiasi cha Tsh. 46,533,363.00.
Vikundi vya wanawake vimeonesha mwitikio mkubwa katika kutekeleza masharti ya mikopo hii yanayowataka kufanya marejesho kwa muda uliopangwa ili na wengine waweze kunufaika na mikopo hii.
Bi Jovitha Juston Mwenyekiti wa Jukwaa la uwezeshaji kiuchumi Wanawake ni mmoja wa akina mama wanaonufaika na mikopo hiyo tangu mwaka 2016, ameeleza kuwa mwanzoni alikuwa akihofia sana suala la mikopo kutokana na namna jamii ambavyo imekuwa ikitafsiri jambo hili kuwa mikopo inapelekea watu wengi kufilisiwa mali zao lakini baada ya kupata elimu kutoka kwa wataalam wa idara ya maendeleo ya jamii ameweza kubadili mtazamo wake na kwa sasa mikopo hii imemuwezesha kuwa na biashara kubwa ya uuzaji wa dagaa ndani ya nchi na nje ya nchi.
Kutokana na utoaji wa mikopo hiyo, Halmashauri ya wilaya ya Muleba ilipata nafasi za ushindi kwa miaka miwili mfululizo kama ifuatavyo; Mwaka 2017/2018 ilipata nafasi ya 5 kitaifa na kutukuniwa cheti cha ushindi na katika mwaka wa fedha 2018/2019 ilishika nafasi ya tatu kitaifa napo pia ikapewa cheti cha ushindi.
Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo utekelezaji wa sheria ya mkopo pamoja na kanuni zake za mwaka 2019 ulivyoanzishwa, Halmashauri iliweza kutoa mikopo kwa thamani ya Tsh. 670,500,000.00 ambapo kwa vikundi vya wanawake 199, vikundi 113 vilikopeshwa Tsh. 266,000,000 kutoka mapato ya ndani na vikundi 86 vilikopeshwa Tsh. 212,555,425.00 kutoka kwenye marejesho (Revolving fund), vikundi vya vijana 53 vilikopeshwa Tsh. 162,444,575.00 ambapo vikundi 51 vya vijana vilikopeshwa Tsh. 145,444,575.00 kutoka mapato ya ndani na vikundi viwili vya vijana vilikopeshwa Tsh. 17,000,000.00 kutoka ofisi ya Waziri Mkuu. Vikundi vya watu wenye ulemavu 10 vilivyokopeshwa Tsh. 29,500,000.00 kutoka kwenye mapato ya ndani.
Bwana Naziru Omary Mwenyekiti wa kikundi cha Nyemenoha kinachojishughulisha na shughuli za kilimo cha matunda na Kahawa, kilichopo Kata ya Magata Karutanga ambacho ni miongoni mwa vikundi vya vijana vilivyopokopeshwa fedha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ameeleza kuwa mkopo umewanufaisha sana vijana kwani wameweza kukua kiuchumi kwa kuzalisha kiasi kikubwa cha matunda ambayo uyauza kwenye viwanda vya kutengeneza juisi.
“Hakika tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuguswa na hitaji la ajira kwa watanzania wengi hususani vijana na hivyo kuanza kutukopesha mikopo isiyokuwa na riba. Wapo vijana wengi mtaani wamemaliza elimu ya chuo kikuu lakini wanakosa mtaji wa kujiari, hivyo nawasihi vijana wenzangu wajiunge katika vikundi, wavisajiri na kisha wakikidhi vigezo vya kukopesheka wakope fedha zitakazowasaidia kujiinua kiuchumi” alieleza Bwana Naziru Omary.
Kutokana na kanuni ya utoaji wa mikopo asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa mchanganuo wa asilimia 40 Wanawake, asilimia 40 Vijana na asilimia 20 watu wenye ulemavu changamoto kubwa inayoikumba Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ni vikundi vichache vya vijana na watu wenye ulemavu kujitokeza kuchukua mikopo kulingana na asilimia zilizotengwa hivyo fedha hizo kubaki kwenye mfuko. Pia urejeshaji hafifu wa fedha zinazokopeshwa vikundi vya vijana na walemavu kuchelewesha marejesho kwa wakati.
Kutokana na changamoto hii Halmashauri kupitia Mkutano wa Baraza wa madiwani ilipitisha azimio la kuwafuatilia kwa karibu na mara kwa mara vikundi vyote vinavyoshindwa kurejesha ili kuhakikisha fedha yote ya Serikali inayokopeshwa inarejeshwa kwa wakati. Aidha, wameendelewa kupewa elimu itakayowasaidia kuendesha biashara zao kulingana na soko la uhitaji ili zisikwame.
Bwana Moses Banoba wa kikundi cha WALEMAVU TUNAWEZA kinachojighulisha na ufundi cherehani kilichopo Kata ya Gwanseli ameeleza kuwa kundi la watu wenye uhitaji maalum ni makundi ambayo jamii iliyasahau kwa muda mrefu kwa kuamini kuwa ulemavu wao hawawezi kufanya shughuli yoyote ya kimaendeleo. Baada ya Serikali kuwapa nafasi wengi wameonesha uwezo na kuwa wanaweza kufanya shughuli za kimaendeleo na sasa wameanza kukopeshwa mikopo isiyokuwa na riba hivyo kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Kwa pamoja vikundi hivi vinatoa pongezi kwa Serikali kwa kuona uhitaji wa kuwezeshwa na kupatiwa mikopo hali ambayo imewainua kiuchumi na kuwawezesha kujikwamua kimaisha. Aidha, wanatoa shukrani kwa Serikali kupitia Halmashauri kwa kuwaamini na kuwapa mikopo isiyokuwa na riba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa