Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Ndg. Emmanuel Sherembi ametembelea na kukagua shughuli za ujenzi na upanuzi wa Kituo cha Afya Kimeya ili kuona maendeleo ya ujenzi huo unaotakiwa kukamilika ifikapo tarehe 31/05/2018.
Akikagua ujenzi huo, Ndg. Emmanuel Sherembi amewasisitiza mafundi waliopewa kazi za ujenzi wa kituo hicho kukamilisha kazi zilizobaki kwa wakati. Na kuwataka wafanye kazi mchana na usiku ili kuhakikisha wanakamilisha ujenzi ndani ya muda waliopewa.
"Zimebaki siku chache mkabidhi kazi hii, tuliona ni vema tuweke umeme ili muweze kufanya kazi mchana na usiku hivyo nategemea nikirudi hapa tarehe 31/05/2018 nitakuta kazi hii imekamilika" alieleza Ndg. Emmanuel Sherembi.
Kituo cha Afya Kimeya ni miongoni mwa vituo 139 vya awamu ya pili ambavyo kila kituo kilipewa kiasi cha shilingi milioni 400 kutoka serikali kuu kwa ufadhili wa World Bank kwa ajili ya upanuzi wa vituo na hadi sasa chumba cha upasuaji (Theatre), Wodi ya Akina mama, Nyumba ya mtumishi, Maabara na Chumba cha kuhifadhia maiti (mortuary) vyote vipo katika hatua ya umaliziaji.
Ujenzi huu umetekelezwa na mafundi wanaopatikana katika maeneo ya wananchi na kila jengo linafundi anayejitegemea ili kusaidia kukamilishaujenzi huu kwa muda uliopangwa. Aidha, ujenzi huu unasimamiwa na Kamati ya Ujenzi iliyotokana na bodi ya Kituo cha Afya kwa kushirikiana na wataalamu kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ambao ni Mhandisi wa Ujenzi, Afisa Manunuzi, Mganga Mkuu na Afisa Mipango.
Ujenzi ulianza mnamo mwezi Februari, 2018 na unatakiwa ukamilike kufikia tarehe 31/05/2018 kama ambavyo Serikali imeagiza.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa