Kiasi cha Tshs Mil. 584 kimetolewa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujenga Shule mpya ya Sekondari Makongora Katika Kata ya Ruhanga, itakayo kuwa na Vyumba nane vya Madarasa,Jengo la Utawala,Maabara tatu, Chumba cha komputa,Maktaba,Kichomea taka pamoja na matundu 20 ya vyoo.
Akiwasili katika eneo la ujenzi Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe.Dkt.Abel Nyamahanga akiambatana na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini Mhe.Charles Mwijage,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bi.Christina Akyoo na baadhi ya Wataalamu wa Halmashauri(CMT)ambao waliungana pamoja kwenda katika kijiji hicho kukagua na kuona eneo la ujenzi wa Shule hiyo ambayo itakwenda kutatua adha ya wingi wa Wanafunzi ambao wanakwenda umbali mrefu kusoma katika Shule ya Sekondari Ruhanga.
Katika kikao kifupi kilichofanyika katika eneo la ujenzi wa Shule, Mhe.Dkt.Abel Nyamahanga amewataka viongozi wa Serikali ya Mtaa na Wananchi wote kuhakikisha wanasimamia Mradi huo ipasavyo na kuhakikisha wanakuwa Walinzi wa Vifaa ambavyo vitaletwa kwa ajili ya ujenzi huo ambao ukikamilika utaifanya Shule hiyo kuwa bora na ya Mfano katika Wilaya ya Muleba.
Aidha Mhe.Dkt.Nyamahanga ameongeza kuwa ni muda muafaka sasa wa kutambua na kuweka mipaka ya kudumu katika eneo hilo kwa kulipima,na hivyo Mkurugenzi Mtendaji aliagizwa kuita wataalamu wa ardhi kupima na kutambua Mipaka ya eneo la Shule hiyo kabla ya watu kuingia ndani ya Mipaka ya eneo hilo.
"Mkurugenzi waite watu wa ardhi waje wapime eneo hili ili tutambue Mipaka yetu yakudumu kuwa inaishia wapi kwani kuna watu wataanza kuingia, hivyo tunataka Shule hii iwe nzuri ya mfano na ya viwango ili watu mjivunie na kuthamini kazi Nzuri inayofanywa na Mhe.Mbunge wetu, Diwani wetu, Chama na kazi Nzuri inayofanywa na Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
Kwa upande wake nae Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini Mhe.Charles Mwijage alitumia muda huo kumshukuru Mhe. Nyamahanga,Mwenyekiti wa Halmashauri,Mkurugenzi Mtendaji pamoja na wataalamu kwa kukubali wazo la ujenzi wa Shule hiyo katika Kijiji cha Makongora ambacho hakikuwa na shule hapo awali.
Imeandaliwa na kutolewa na;
Eusebius J. Kiluwa
KAIMU MKUU KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa