Samaki aina ya Sangara kilo 400 wenye thamani ya fedha za kitanzania TSH.4000,000 waliovuliwa chini ya kiwango cha sheria ya uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 waliokuwa wakisafirishwa kutoka mwalo wa wa Ruhanga uliopo kata ya Magata Karutanga wilaya ya Muleba kuelekea wilaya ya Karagwe wamekamatwa leo Agost 13 majira ya saa 10 jioni na Mkuu wa wilaya ya Muleba, Mh. Toba Nguvila akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Mkuu wa wilaya ameeleza kuwa hivi karibuni kamati ya ulinzi na usalama imeteua kikosi kazi kikijuisha wataaalamu wa sekta ya uvuvi kutoka ofisi ya Mkurugenzi na taasisi zingine za Serikali zinazosimamia shughuli za Ulinzi na Usalama
"Nawasihi sana wavuvi na wafanyabiashara kuacha mara moja biashara ya uvuvi haramu kwani Serikali ipo kazini na haita mvumilia mtu yeyote ambaye anajihusisha na shughuli za uvuvi haramu zinazosababisha uharibifu wa raslimali za taifa. Endapo samaki hawa wangevuliwa katika kiwango kinachostahiri wangekuwa na tani nyingi na tani hizo zingeingizia pato kubwa kwa taifa" ameeleza Mhe. Toba Nguvila.
Watuhumiwa waliokamatwa ni waendesha bodaboda watatu ambapo bodaboda wawili ni kutoka kijiji cha Rubya na kwa mujibu wa watuhumiwa hawa wameeeleza kuwa wametumwa na wafanyabiashara kupeleka samaki hao.
Aidha, Mkuu wa wilaya ameeleza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu huku akiwataka viongozi waliopo mwambao wa ziwa Victoria kuendelea kutoa ushirikiano ili kudhibiti uvuvi haramu katika wilaya. Pia amewaonya waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda wanaotumika kusafirisha samaki zisizokidhi viwango kuacha kujihusisha na shughuli hiyo ya uvuvi haramu kwani wamekuwa chanzo cha kutorosha samaki hao kwenda nje ya Wilaya na hadi nje ya nchi.
Naye Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Muleba Bw. Wilfred Tibendelana amesema wataendelea kudhibiti uvuvi haramu kwani hawatomfumbia macho mvuvi au mfanyabiashara yeyote atakayehusika na uvuvi haramu na kusababisha kushuka kwa mapato ya Halmashauri.
Watuhumiwa hao waliokamatwa watafikishwa Mahakamani na watashtakiwa kwa sheria za nchi zilizowekwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa