Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera William Mwampaghale amewaagiza Watendaji Kata kushirikiana na Askari wa Kata kuwaelimisha wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi ili kuweza kupunguza vitendo vya mauaji Wilayani Muleba.
Akizungumza katika Kikao hicho kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera amewahimiza Watendaji wa Kata kuwashirikisha viongozi wa Kimira pamoja na viongozi wa Kidini kutoa elimu kwa wananchi ili vitendo vya mauaji viweze kukomeshwa Wilayani Muleba.
"Mnavyoenda kufanya mikutano kwenye maeneo yenu washirikisheni na viongozi wa Kimira kiongozi wa kimira atatoa elimu hata kwa kilugha wananchi watamuelewa jambo ambalo linaweza kusaidia kwa wananchi hawa kuacha kuuana" amesema William Mwampaghale.
Lakini pia amewaagiza maafisa mifugo kutoa elimu kwa wafugaji kufuga kisasa kwa kuhakikisha kiwango cha mifugo waliyonayo inaendana na eneo la ufugaji lililopo ili kuweza kupunguza migogoro ya wafugaji na wakulima.
Sambamba na hayo amewahimiza wafugaji kuhakikisha wanawaajiri wachungaji wa mifugo na walinzi wa mifugo yao wanaowafahamu pamoja na kuhakikisha wanajenga mazizi yanayofaa kufugia mifugo yao ili kuweza kupunguza tatizo la wizi wa mifugo.
Wakati wa Ufunguzi wa Kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dkt Abel Nyamahanga ameeleza kuwa migogoro ya ardhi imekuwa chanzo cha mauaji pamoja na imani za kishirikina hivyo ameshauri kuwa ni vema wananchi wakawa wavumilivu wakaacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi pamoja na kuheshimu utawala wa sheria ili kuweza kuondokana na vitendo vya mauaji Wilayani Muleba.
Naye Mkuu wa Sehemu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Ndg. Charles Ntaki Mayunga ameeleza kuwa mfugaji anapopeleka mifugo yake kuuza kwenye mnada ni lazima awe na barua ya utamburisho kutoka kwa Mtendaji wa Kata au Mtendaji wa Kijiji kama mamlaka ambazo zinatambulika kusimamia ulinzi na usalama katika eneo husika na mmuzi akishanunua mifugo lazima atapewa kibari ambacho atakitumia mpaka sehemu anayopeleka mifugo hiyo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera ameeleza kuwa kwa mwaka jana yameripotiwa mauaji ya watu 16 kwa Wilaya ya Muleba na kwa mwaka huu kuanzia mwezi wa kwanza hadi sasa tayari yameripotiwa mauaji ya watu 15 na kwa wizi wa mifugo mwaka jana yarilipotiwa matukio 15 na kwa mwaka huu tayari yameripotiwa matukio 30.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa