Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus amekabidhi vishikwambi kwa Wakuu wa Sehemu na Wenyekiti wa Kamati ili viweze kusaidia kupunguza gharama za kusafirisha nyaraka pamoja na urahisishaji wa shughuli mbalimbali.
Akizungumza baada ya kukabidhi Vishikwambi hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri amesema kuwa vishikwambi vitaweza kupunguza gharama za kutoa nakala za makaburasha, kupunguza gharama za usafirishaji wa makaburasha, kusaidia kupata taarifa za vikao kwa wakati pamoja na kurahisisha utendaji wa kazi mbalimbali za Halmashauri.
"Ushauri wangu kwenu Wakuu wa Sehemu na Wenyeviti wa Kamati hakikisheni mnavitunza vizuri vishikwambi hivi na hakikisheni mnaongeza morali ya utendaji wa kazi unaostahili na nina imani kwamba vitatumika kama ilivyopangwa ili tuweze kutimiza malengo ya Halmashauri yetu" amesema Mhe. Magongo Justus.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Stewart Mtondwa ameeleza kuwa Jumla ya vishikwambi vilivyonunuliwa ni vishikwambi 25 ambapo vishikwambi 18 vitatumiwa na wakuu wa Idara na vishikwambi 7 vitatumiwa na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu na vyote kwa pamoja vimegharimu kiasi cha Tsh. Milioni 37,250,000/=
Naye Bi. Enelietha Wiliamu ambaye ni Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Jamii ameeleza kuwa hapo awali kulikuwa na changamoto kupata makaburasha kwa wakati na gharama zilizokuwa zinatumika zilikuwa kubwa hivyo vishikwambi hivyo vitaweza kurahisisha utendaji kazi na majukumu ya kiofisi kwa ujumla wake.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa