Kufuatia kukamatwa kwa samaki wachanga aina ya Sangara maarufu kwa jina la (Kayabo), katika kijiji cha Rubili kata ya Mazinga, Wilaya ya Muleba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba amewasimamisha kazi na kuwafikisha mahakamani Mtendaji wa Kata Ndg. Crispinius Mukyanuzi, Mtendaji wa Kijiji Ndg. Medard Kalugendo na Afisa Uvuvi wa Kata, Ndg. Emmanuel Mabau kwa kosa la kushindwa kusimamia majukumu yao ya kudhibiti uvuvi haramu
Kutokana na agizo la Waziri mwenye dhamana, Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Mhe. Luhaga Mpina (MB) aliyoitoa Mkoani Kagera akiwa katika ziara yake mwishoni mwa mwezi Desemba 2017, juu ya Udhibiti wa Uvuvi Haramu uamuzi huu umefikiwa baada ya watendaji hawa kukiuka sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 kifungu cha 45, 3a, b na kanuni za uvuvi za mwaka 2009 kifungu cha 58 (a). Aidha Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa kitongoji cha Rubili, Mwenyekiti na Katibu wa BMU Kijiji Rubili nao wamekamatwa na watafikishwa mahakamani sambamba na watendaji hao.
"Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga kutokomeza uvuvi haramu hivyo ninawakumbusha na kuwasisitiza sana watendaji wote wa serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kusimamia Sheria, Taratibu na Kanuni katika kutekeleza majukumu." alieleza Ndg. Emmanueli Sherembi.
Mwisho amewaomba wananchi kutoa taarifa kwa viongozi na vyombo vya ulinzi na usalama pindi wanapobaini kuna uvuvi haramu katika maeneo yao na kuwasihi kuacha kujihusisha na uvuvi haramu utakao wapelekea wafikishwe mahakamani na kufungwa.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa