Halmashauri ya Wilaya ya Muleba katika Mkutano wake wa Baraza la Robo ya nne April-Juni, 2021/2022 kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Idara/Sehemu, imejipanga kuongeza hali ya ufaulu wa kidato cha nne kama ambavyo Wilaya inafanya vizuri katika ufaulu wa kidato cha sita.
Akizungumza kwenye Mkutano huo wa Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Magongo Justus Magongo ameeleza kuwa ni kweli iko haja ya kuwa na mikakati ya kupandisha hali ya ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi kidato cha nne ili matokeo yawe mazuri kama yalivyo matokeo ya kidato cha sita.
“Kama ambavyo mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini ameeleza, tunaipongeza Idara ya Elimu Sekondari kwa ufaulu wa kidato cha sita, wanafunzi wamefaulu vizuri, sasa ni wakati kuwa na mikakati na kuhakikisha ufaulu huu uwe na kwa kidato cha nne pia. Najua tukijipanga tunaweza”, ameeleza Mhe. Magongo.
Akitoa hoja hiyo, Mhe. Dr. Oscar Kikoyo, mbunge wa jimbo la Muleba Kusini ameipongeza idara ya Elimu Sekondari kwa ufaulu wa kidato cha sita na kueleza kuwa ufaulu wa daraja la kwanza ni asilimia 27, ufaulu wa daraja la pili ni asilimia 56.45, ufaulu wa daraja la tatu ni asilimia 16 na hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la nne wala sifuri hivyo jitihada na nguvu kwa sasa ielekezwe kwa kidato cha nne. Na kueleza namna wabunge walivyojipanga kuwapa motisha walimu kwa shule zinazofanya vizuri.
Naye Mhe. Charles Mwijage, mbunge wa Muleba Kaskazini ameeleza kuwa tayari ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023 umeanza ikiwa sambamba na ujenzi wa shule mpya, huku akimtaka Mkurugenzi kujiandaa na umaliziaji wa maboma kwani fedha zote za mfuko wa jimbo zitakwenda kununua saruji kwa ajili ya ujenzi huo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Ndg. Evart Kagaruki alieleza kuwa ni jambo jema kuwa na mikakati ya kuinua ufaulu wa kidato cha nne. Hivyo suala hilo limepokelewa, wataalam watakaa na kuja na mikakati itakayowezesha kuinua kiwango cha ufaulu kwa kidato cha nne.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya la Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa