Katika jitihada za kuboresha mazingira ya watumishi, hususani walio katika mazingira magumu Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kupitia Idara ya Elimu Msingi, imetoa pikipiki tatu kwa walimu wakuu wa shule za msingi Byengerere, Rutoro na Kyarutare zilizopo kata Rutoro kilometa 78 kutoka makao makuu ya Wilaya.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi pikipiki hizo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus amesema kuwa Halmashauri inaendelea kuboresha mazingira ya watumishi kwa kuwapa motisha na kuwarahisishia katika majukumu yao ili waweze kutoa huduma stahiki.
“Ni matarajio yangu pikipiki hizi zitafanya kazi iliyokusudiwa sitarajii pikipiki hizi kwenda kufanya biashara ya kubeba abiria maarufu kama bodaboda. Ni vifaa vilivyonunuliwa kwa gharama kwahiyo utunzaji ni suala la msingi. Mwalimu utakayetumia utumie kwa malengo ya uendelevu ili zidumu”, ameeleza Mheshimiwa Magongo
Aidha, ameishukuru jamii ya wana Muleba, kwani kupitia ushuru unaokusanywa kwao umewezesha kununua pikipiki hizo. Ameendelea kueleza kuwa fedha ya mapato ya ndani inayokusanywa inafanya mambo makubwa kama hayo kwani wiki iliyopita zilikabidhiwa pikipiki tatu kwa maafisa mifugo wa kata za Kamachumu, Muhutwe na Kishanda. Na Halmashauri itaendelea kuboresha mazingira ya kazi ya watumishi kila mwaka kadri fedha inavyopatika.
Akiwasilisha taarifa fupi ya makabidhiano ya pikipiki hizo, Kaimu Afisa Elimu Awali na Msingi, Ndugu Titus Sudi Amour ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kupitia Sehemu ya Elimu ya Awali na Elimu ya Msingi ilibaini changamoto ya usafiri kwa walimu wa shule za Msingi Kata ya Rutoro na kuona ipo haja ya kuwanunulia pikipiki zitakazowawezesha katika majukumu yao.
Aina ya pikipiki zilizonunuliwa ni Honda CC 125, zenye thamani ya jumla ya Tsh. milioni 10.5 sawa na Tsh. milion 3.5 kila moja pamoja na ongezeko la thamani (VAT). Na pikipiki hizo ni mali ya shule.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa