Katika ziara ya zoezi la kudhibiti uvuvi haramu Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amewaomba viongozi wakiwemo Watendaji wa Kata, Wenyekiti wa Vijiji na Vitongoji pamoja na viongozi wa BMU kuhakikisha wanadhibiti uvuvi haramu alipofanya ziara hiyo katika Kata ya Rulanda na Gwanseli wilayani Muleba.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya ya Muleba ametoa onyo kwa viongozi hao kuwa endapo ikibainika kwenye maeneo yao kuna wavuvi wanaotumia dhana haramu katika maeneo yao bila wao kutoa taarifa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
"Uvuvi wa kutumia timba makokoro, katuri, katwange, taa zenye mwanga mkali, boti na mitumbwi ambayo haijasajiliwa ni uvuvi ambao unaharibu ajira, ni uvuvi ambao unaharibu rasirimali za viwandani na ajira viwandani, ni uvuvi unaoharibu hata biashara za akina mama pamoja na kuikosesha mapato Halimashauri kwahiyo niwaombe kuacha uvuvi haramu" amesema Mhe Toba Nguvila.
Aidha, Mkuu wa wilaya amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale watakapokuwa wanaona shughuli za uvuvi haramu zikiendelea kufanyika katika ziwa ili kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika na vitendo hivyo.
Kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya ya Muleba Ndg. Greyson Mwengu amewaeleza viongozi wa BMU wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watendaji kuwa wakisimamia vizuri uvuvi haramu utakoma katika maeneo yao.
Lakini pia amewaomba viongozi hao kuwa na oparesheni zao za kufanya zoezi la kudhibiti uvuvi haramu kwa kuhakikisha wanatoa taarifa pale wanapobaini kuwa kuna uvuvi haramu katika maeneo yao ili kuweza kukomesha uvuvi haramu wilaya ya Muleba.
Naye Kaimu Afisa uvuvi wa wilaya ya Muleba Ndg. Ignasio Rwina amewaeleza wananchi kuwa kwa mujibu wa Sheria za uvuvi uvuvi wa kutumia makokoro, timba na nyavu zenye macho madogo haviruhusiwi kutumika kuvua samaki na kuwaeleza kuwa nyavu zinazoruhusiwa ni kuanzia nchi sita kwenda juu hivyo amewaomba viongozi kutoa elimu kuwaelezea wananchi madhara ya dhana hizo .
Mkuu wa wilaya pamoja na kamati ya usalama amefanya ziara hiyo katika kata ya Rulanda na kata ya Gwanseli kijiji cha Misikilo.
Imeandaliwa na Kutolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa