Katika Kikao kilichofanyika ndani ya Ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Watendaji wa Kata wamesaini mikataba ya kufikia malengo ya makusanyo ya kiasi cha Tsh.Bilioni 10 kwa Mwaka wa fedha 2023-2024.
Akizungumza na Watendaji hao Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Dtk. Peter Nyanja amewaeleza Watendaji kuwa wakikusanya na kuvuka malengo ya makusanyo watasaidia upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi kwa wananchi pamoja na stahiki za kiutumishi.
"Twende tukafanye kazi na inawezekana tuwafikishieni taarifa hizi Waheshimiwa madiwani pamoja na wananchi kwa kuitisha mikutano ma kufanya vikao vya dharula ili Waheshimiwa madiwani waweze kuyajua malengo ya makusanyo tuliyojiwekea kwa mwaka huu wa fedha" amesema Dkt Peter Nyanja.
Naye Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Yonas Charugamba amesema kuwa kwa wanaosafirisha ndizi wasifunge ndizi hizo kwa sababu imebainika kuwepo kwa changamoto ya upotevu wa mapato pale ndizi inapokatiwa ushuru ikiwa imefungwa na kudhaniwa kuwa ni ndizi moja kumbe ndani yake kuna ndizi mbili hivyo amewahimiza Watendaji kuzuia kukatia ushuru ndizi ambazo zimefungashwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Utumishi Bi. Christina Akyoo amewahimiza Watendaji wa Kata wanapowakaimisha nafasi ya Utendaji wa Vijiji Maafisa Ugani na Maafisa Maendeleo ya Jamii barua za kukaimishwa zitoke katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Sambamba na hayo amewahimiza Watendaji wa Kata kuwa Mtendaji wa Kijiji anapokuwa likizo akaimishwe mtendaji wa kijiji Jirani mpaka Mtendaji wa Kijiji husika atakapokuwa amemaliza likizo yake.
Kaimu Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Fidelis Mugarula Kyabona amewahimiza Watendaji kuwashirikisha viongozi kuanzia ngazi za vitongoji kubuni vyanzo vya mapato kutoka katika ngazi za chini ili viweze kujadiliwa na kutengeneza Sheria ndogo za vyanzo hivyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa