Kutokana na mvutano uliokuwepo baina ya viongozi wa Kata ya Rulanda na viongozi wa Kata ya Bisheke uliotokana na mradi wa maji Kyamyorwa unaohudumia kata ya Kasharunga na Kata ya Rulanda, ambapo tanki la Kata ya Rulanda kujengwa katika kijiji cha Bisheke huku Bisheke ikiwa si mnufaika wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amefika na kutatua mgogoro huo kwa kumuagiza Mkandarasi kujenga vituo vitatu vya kuchotea maji katika vitongoji vya Kata ya Bisheke vinavyopakana na eneo ambalo tanki la maji linajengwa.
Akizungumza mara baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, ameeleza kuwa hakuna haja ya kuvutana maana miradi ya maendeleo ni ya waTanzania wote hivyo kumtaka Meneja wa Maji Vijijini kumuelekeza mkandarasi kujenga vituo vitatu vya kuchotea maji kwa kitongoji cha Ichwandimi, Kabuga na Nyakahanga vya kata ya Bisheke ili wananchi wa maeneo hayo nao wanufaike na mradi huo.
"Nimefika eneo la mradi na kujionea hali halisi, sioni sababu ya kuendelea kuvutana nakuagiza Meneja wa RUWASA, muelekeze Mkandarasi, vituo vitatu kati ya vituo kumi na tatu vinavyojengwa katika mradi huu vijengwe katika vitongoji vya Kijiji hiki mahali ambapo tanki la maji linajengwa. Haitakuwa busara tanki la maji linajengwa hapa Kata ya Bisheke lakini mradi unakwenda kuhudumia kata ya jirani ya Rulanda na wakati huohuo wananchi wa eneo hili wanahitaji huduma ya maji, hivyo vituo vitatu vya kuchotea maji vijengwe kata ya Bisheke na zile vituo 10 ndio vikahudumie kata ya Rulanda", ameeleza Mhe. Nguvila.
Aidha, ameagiza kuwa mama mwenye eneo ambapo tanki la maji linajengwa alipwe fidia ya mazao yake yaliyoondolewa kupisha ujenzi wa tanki. Huku akielekeza mradi utakapokamilika bei ya ndoo ya maji isizidi shilingi 50 na kuwasisitiza wananchi kuwa mradi utakapokamilika wahakikishe wanaulinda mradi huo bila na si kufanya uharibifu.
Kwa upande wa Madiwani wa Kata ya Bisheke Mhe. Alexander Petro na Kata ya Rulanda Mhe. Evart Tiletwa wamemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufika kuona hali halisi, kuzungumza na viongozi na kutoa maelekezo ambayo yameafikiwa na pande zote mbili huku jina la Mradi likibaki kama lilivyo Mradi wa maji Kyamyorwa.
Naye Mhandisi Kaiza Zephline Kaimu Meneja RUWASA Wilaya ya Muleba ameeleza kuwa mradi huo umetengewa bajeti ya kiasi cha Tsh. Bilioni 3.2 na mradi huo utatekelezwa na Mkandarasi Mbeso Engineering kutoka Dar es Salaam ulianza kutekelezwa tarehe 24/05/2022 na unatarajiwa kukamilika tarehe 25/11/2022.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa