Katika Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika lkatika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Katibu Tawala wa Wilaya Ndg. Greyson Mwengu amewaagiza Madiwani kutoa ushirikiano katika maeneo yao ili uvuvi haramu uweze kutokomezwa.
Akizungumza katika Baraza hilo Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba amesema kuwa endapo viongozi watashindwa kusimamia na kupambana na uvuvi haramu jambo hilo litapelekea kuadimika kwa samaki katika Wilaya ya Muleba hivyo ni vema viongozi wakiwemo madiwani, watendaji wa kata na vijiji pamoja na wenyekiti wa vijiji kuhakikisha wanatoa ushirikiano kupambana na uvuvi haramu kuhakikisha unakomeshwa katika Wilaya ya Muleba.
"Kama unafanyika uvuvi haramu na kiongozi ukaonekana unautetea mwisho wa siku samaki wataisha yatabakia tu maji ya kuoga na kupikia na siku samamki wakiisha wananchi watayahamishia hayo madhambi kwako na kusema kuwa wewe kiongozi sio mzuri kama umishindwa kusimamia na kuhakikisha unapambana na uvuvi haramu" amesema Ndg. Greyson Mwengu.
Aidha. Katika Baraza hilo amewaomba madiwani kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu sana ujenzi wa madarasa yanayojengwa kwa sasa katika maeneo yao ili madarasa hayo yaweze kukamila kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili ili kufikia tarehe 25 madarasa yote yawe yamekamilika.
"Madiwani na nyie kwa nafasi yenu mpite katika hivyo vyumba vya madarasa mkague na kuelekeza kama sisi tunavyopita na kuelekeza na nyie fanyeni hivyo ili ujenzi wa madarasa uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa" ameongeza Ndg. Greyson Mwengu.
Sambamba na hayo amewaagiza madiwani kuwahimiza wananchi kuendelea kulima mazao ya chakula kwa kuweka akiba ya vyakula ili kuweza kukabiliana na janga la uhaba wa vyakula katika Wilaya ya Muleba.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Muhaji Bushako amesema kuwa ni vyema madiwani wakahakikisha wanatoa ushirikiano wa kupata majina ya mialo ambayo inashiriki katika uvuvi haramu na kufika katika mialo hiyo kujionea ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa watu wanaofanya vitendo hivyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Stewart Mtondwa amesema kuwa kwa mtu atakayemuona mvuvi anayefanya uvuvi haramu kwa kutega samaki bila kutumia nyavu zinazostahili ni vizuri akatoa taarifa kwa uongozi wa Halmashauri na jeshi la polisi ili kuweza kunusuru na kukomesha uvuvi haramu.
"Hayo yote tukiyafanya kwa pamoja viongozi katika ngazi ya Kata, ngazi ya Tarafa na ngazi ya Wilaya wakiwemo pia waheshimiwa madiwani tunahitaji kushikiana kwa pamoja kuhakikisha uvuvi haramu unatokomezwa katika Wilaya yetu" amesema Ndg. Stewart Mtondwa.
Diwani wa Kata ya Biilabo Mhe. Beatus Mussa ameshauri kwa kusema kuwa ni vema wananchi wakapanda mazao ya mda na kuhifadhi chakula ili chakula hicho kiweze kuwasaidia kupambana na uhaba wa chakula na hata kuwasaidia maeneo mengine ambayo yanaweza kukumbwa na changamoto hiyo.
Akizungumzia suara la uvuvi haramu amesema kuwa ni vyema kwa kata ambazo zinapakana na ziwa wahamasishe wananchi wao waweze kuachana kabisa na uvuvi haramu ambapo amesema kuwa uvuvi haramu unaharibu hata mazalia ya samaki jambo ambalo linaweza kuhatarisha uchumi wa uvuvi katika maeneo yetu.
Naye Pastory Gwanchele Diwani wa Kata ya Nyakabango ameeleza kuwa ni vema Maafisa uvuvi wakatoa elimu kwa wavuvi wadogo wadogo kuhusiana na madhara ya uvuvi haramu ili waweze kuachana na uvuvi haramu jambo ambalo litasaidia kupuguza uvuvi haramu Katika Wilaya ya Muleba.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa