Katika Kikao kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dkt Abel Nyamahanga amewahimiza Maafisa Ugani Kutoa elimu kwa wananchi kuzitumia njia za kisasa katika Kilimo,Uvuvi na Ufugaji ili waweze kuondokana na umaskini.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya amewahimiza Maafisa Ugani Kushirikiana na Watendaji wa Kata, Watendaji wa vijiji pamoja Wenyeviti wa Vijiji kuitisha mikutano ili wananchi waweze kupatiwa elimu kuhusiana na umuhimu wa kulima, kufuga na kuvua kisasa ili waweze kuzalisha mazao yenye ubora.
"Twende tukawahudumie wananchi, twende tukawakomboe wananchi kutoka katika dimbwi la umasikini, twende tuwaelimishe wananchi wawe na uwezo wa kujitegemea wapate chakula cha kutosha ili tuweze kupata lishe na kuongeza pia mapato ya Halmashauri" amesema Mhe. Dkt Abel Nyamahanga.
Aidha, amewasihi Maafisa Ugani wa Kilimo na Mifugo kuwafikia wananchi katika maeneo yao ili kuweza kuwasaidia kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Sehemu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Ndg. Charles Ntaki Mayunga ameleza kuwa hadi sasa wameendelea kuwajengea uwezo Maafisa Ugani kupitia programu mbalimbali ambapo amesema kuwa ipo programu ya ufufuaji na uendelevu wa zao la kahawa aina ya robusta kupitia mradi wa (CAFE AFRIKA) kaskazini magharibi mwa Tanzania hivyo kupitia programu hiyo tayari Wagani 30 wameshapatiwa mafunzo na tayari huko vijijini yapo mashamba ya mfano zaidi ya 30.
Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Muhutwe Ndg. Paul Kakoko amehaidi kuwa kwa upande wa kilimo watahakikisha wanahamasisha wakulima kulima mazao ambayo yatachangia kuondoa utapiamulo pamoja na kuwazungukia wananchi kutoa elimu kuhusiana na kulima kufuga na kuvua kwa tija ili wananchi waweze kuinuka kiuchumi na kupata lishe iliyo bora.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa