Katika Kikao cha Baraza la Wafanyabiashara kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Kemirembe Rwota amewasihi maafisa Biashara kuwatembelea wafanyabiashara ili kubaini na kutatua changamoto walizonazo.
Akizungumza katika Kikao hicho Mkuu wa Wilaya amesema kuwa ni vema Maafisa Biashara wasiishie kufanya kazi maofisini wafike hadi kwa wafanyabiashara ili waweze kujua changamoto zao na kumsisitiza Mkurugenzi kuhakikisha anafuatilia kujua kama hayo yanafanyika.
"Mnaweza mkawa mna desturi ya kuwatembelea wafanyabiashara lakini kama mnawatembelea mala moja kwa mwaka mnakuwa hamjatimiza majukumu hata kama wana changamoto zao wanataka kuwaelezea wanakosa pa kuwapata hivyo nadhani tutoke tuwatembelee wafanyabiashara mpaka kwenye maeneo wanakofanyia biashara zao" amesema Mhe. Kemirembe Rwota.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Stewart K. Mtondwa amesema kuwa waendesha bodaboda kupata leseni ni kitu cha msingi sana ambacho kitawasaidia kuendesha shughuli zao ambapo ameeleza kuwa kama wakiwezeshwa wakapata leseni Halmashauri pia inaweza kupata mapato na biashara yao yao ya Bodaboda ikawa halali.
Naye, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Dickson Mnyaga ameeleza kuwa kutokana na wananchi wa Wilaya ya Muleba kujishughulisha na shuguli za Kilimo,Uvuvi na Ufugaji malighafi zinazotokana na shughuli hizo ni kichocheo kikubwa cha kuanzisha viwanda mbalimbali ndani ya wilaya ambapo mpaka sasa wilaya ina viwanda vya vya kati 64 vinavyochakata mazao ya kilimo ikiwa ni pamoja na viwanda vya kukoboa na kusaga kahawa, kukoboa na kusaga unga na kufungasha unga, kukoboa mpunga na kufungasha kwa madaraja.
Kanga Makusi meneja wa Benki ya NMB Muleba ameshauri kurasimisha shughuli ndogondogo zilizopo maeneo ya vijijini na mjini ambapo amesema kuwa wilaya ingeweza kuongeza mapato kama ingetafutwa namna nzuri ya kuwatambua na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo.
Meneja wa TRA Daniel Makirikita Wilaya ya Muleba amesema kuwa sio wafanyabiashara wote wanaoitakiwa kuwa na mashine za EFD kwa wafanyabiashara wanaotakiwa kuwa na mashine za EFD kisheria mauzo yao yanatakiwa kuwa Tsh. milioni 11 na kuendelea na wafanyabiashara wenye mauzo pungufu ya hapo wanatakiwa kuwa na kitabu cha kawaida cha kutoa lisiti kwa wateja.
Naye Khalfan Abubakari Mwenyekiti wa jumuiya ya Wafanyabiashara Wilayani Muleba amesema kuwa ili kuweza kufikia malengo ya makusanyo ya mapato ya Halmashauri ni vema ikatafutwa namna ya kuwakuza wafanyabiashara au kuanzisha biashara mpya au kutengeneza miradi mingine mipya ili kuweza kuyafikia malengo bila kuwaumiza wananchi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa