Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imeendelea kutekeleza mkakati wa kuhama kutoka katika Mfumo wa Uendeshaji wa vikao kwa kutumia Makabrasha na kuanza kutumia Vishikwambi kwa lengo la kuweza kurahisisha na kupunguza gharama za uendeshaji wa vikao vyao.
Jumla ya Vishikwambi 60 vilivyonunuliwa na halmashauri ya Wilaya ya Muleba vimegawiwa kwa Wahe.Madiwani kwa lengo la kuwasaidia kuendesha Shughuli za vikao kwa kupata taarifa na kuzipitia kwa njia ya kimtandano ili waweze kuondokana na changamoto ya utumiaji wa Makbrasha.
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kujadili taarifa za Robo ya pili uliofanyika ndani ya ukumbi wa Halmashauri Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus amewahimiza Waheshimiwa Madiwani kutunza Vishikwambi walivyokabidhiwa ili viweze kutumika kwa matumizi yaliyolengwa.
"Vishikwambi hivi vimetumia gharama kubwa kuvinunua na mpango wake sio wa miezi miwili wala miezi mitatu kwahiyo niwahimize kila mtu akitunze na akitumie kwa matumizi yaliyokusudiwa na sio kwa matumizi mengine" amesema Mhe. Magongo Justus.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha TEHAMA Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Remmy Kaaro amewaeleza Waheshimiwa Madiwani kuwa ni vema wakavichaji kwanza vishikwambi vyao kabla ya kuvitumia na endapo ikitokea kishikwambi kimepata hitilafu amewahimiza kuwasilana na yeye ili kuweza kutatua changamoto hiyo.
Diwani wa Kata ya Mazinga Mhe. Edibily Alex amesema kuwa hapo awali kipindi wanatumia Makaburasha walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutopata Makaburasha kwa wakati kutokana na umbali wa maeneo hasa kwa Kata za Visiwani lakini kupitia Vishikwambi wataweza kupata taarifa za vikao kwa wakati na kuweza kupata muda wa kutosha wa kupitia taarifa kabla ya kujadiliwa kwenye vikao.
kwa upande wake Mhe. Devotha Katabalwa Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Ijumbi ameeleza kuwa kwa kawaida huwa wanatakiwa kupitia Makaburasha ndani ya siku saba kabla ya Vikao vya Baraza hivyo kupitia Vishikwambi hivyo wataweza kupata taarifa hizo na kuzipitia kwa wakati tofauti na awali walipokuwa wanatumia Makaburasha.
Imeandaliwa na kutolewa na;
Eusebius J. Kiluwa
KAIMU MKUU KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa