Katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kiwilaya katika Ukumbi wa Suzana Hotel Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba Ndg. Greyson Mwengu amewasihi wananchi kujitokeza kupima kwa hiari maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili waweze kujua hali ya afya zao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba amesema kuwa ni vema watu wakajitokeza kupima virusi vya UKIMWI hasa wanaume ambao bado mwitikio wao ni mdogo katika upimaji jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za serikali na wadau dhidi ya mapambano ya virusi vya UKIMWI.
"Wanawake mnajitokeza kwa wingi kujua afya zenu kuliko sisi wenye jinsia ya kiume nichukue fursa hii kuwahimiza wanaume wote hebu na sisi tujitokeze kupima afya zetu kwa sababu kupima afya ni hatua moja wa kuweza kujiimarisha kiafya mala baada ya kujua afya yako ikoje" amesema Ndg. Greyson Mwengu.
Lakini pia amesisitiza wanawake wajawazito ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI ni vema wakazitumia kikamilifu huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kwa wale ambao wameshapata maambukizi ya virusi vya UKIMWI na wameshaanza kutumia dawa za ARV wazingatie matumizi sahihi ya dawa hizo na kuzingatia lishe bora ili kuimalisha afya zao.
Sambamba na hayo amewasihi wananchi kuhakikisha wanatoa ushirikiano katika kuthibiti vitendo visivyozingatia usawa na kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu kama ukatili wa kijinsia unaopelekea maambukizi mapya ya VVU.
Kwa upande wake Mratibu wa shughuli za kuzuia maambukizi ya UKIMWI ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Muleba Bi. Enelietha Wiliamu amesema kuwa Wilaya inaendela na mikakati ya kuhakikisha elimu inatolewa kwa makundi lika yakiwemo makundi ya vijana na hata kwa wale aambao wananishi na VVU ili nao pia wawe mabalozi katika jamii kuhakikisha wanatoa elimu katika jamii kuhusu suala zima la kupambana na VVU.
Naye Diwani wa Kata ya Muleba ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Muhaji Bushako ameeeleza kuwa umri wa vijana ndio wapo kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU hivyo ni vema vijana wakahakikisha wanajizuia kutoshiriki Ngono zembe ambazo ndio zinapeleka vijana waliowengi kupata maambukizi ya VVU.
Elivitha Bejumla Greysheni amesema kuwa kwa watu ambao wanaishi na maambukizi ya VVU ni vema wasinyanyapaliwe bali wapewe haki za msingi kama watu wengine maana wakinyanyapaliwa inaweza kusababisha kuhatarisha maisha ya mtu anayeishi na maambukizi ya VVU kama kuchukua hatua za kujiua au kuwa na msongo wa mawazo
Katika taarifa iliyosomwa na Mratibu wa Huduma za Uzani Bi. Dovotha Rutayugo ameeleza kuwa katika kuhakikisha wanapunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni muhimu mjamzito na anayenyonyesha mwenye maambukizi ya VVU kuhakikisha anatumia dawa za kufubaza virusi kwa usahihi, kufanya kipimo cha utambuzi wa virusi katika damu, kujifungua katika kituo cha kutolea huduma za afya na mtoto atakayezaliwa apewe dawa kinga za kumlinda asiweze kupata maambukizi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa