Wakala wa Maji Vijijini RUWASA wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera imefanya ukarabati wa kawaida katika miradi mitatu mikubwa ya maji ambayo ni mradi wa maji Kasharunga uliopo kijiji Kasharunga, kata ya Kasharunga, mradi wa maji Ruteme uliopo kijiji Ruteme na mradi wa maji Kyota uliopo kijiji cha Kyota, Kata ya Kimwani.
Akikagua miradi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila ameagiza kamati zote za maji wilaya ya Muleba kuhakikisha wanawake walinzi kwenye vyanzo vya maji ili kulinda miundombinu ya maji na kuondoa madhara ya uharibifu wa vyanzo vya maji inayoweza kuathiri watumiaji maji.
"Serikali inatumia fedha nyingi sana kujenga na kuendeleza miradi hii, hivyo ni jukumu la wananchi kuitunza na kuendeleza kwa manufaa yao na vizazi vijavyo. Hivyo naagiza kuanzia sasa kila chanzo cha maji lazima kiwe na mlinzi ili kuepukana na changamoto ya kupotea kwa miundombinu ya maji ambayo inahujumiwa na watu ambao hawana nia njema na uwekezaji wa Serikali" ameeleza Mhe. Toba Nguvila.
Maagizo hayo ameyatoa baada ya kutembelea miradi hiyo na kukuta katika miradi yote mitatu hakuna mlinzi hata mmoja kwenye vyanzo vya maji. Aidha, amezitaka kamati za maji mradi wa Rutema na Kyota kupunguza gharama za uuzaji maji kutoka shilingi 100 kwa ndoo moja hadi shilingi 50 kwa ndoo ili kila mwananchi aweze kutumia huduma hii muhimu ya maji kutokana na baadhi ya wananchi kuendelea kuchota maji katika mto kwa kukosa fedha za kununua maji kwa maelezo kuwa gharama zipo juu ya uwezo wao.
Kwa upande wa Meneja wa wakala wa usambazaji maji vijijini (RUWASA) Wilaya ya Muleba, Mhandisi Patrice Jerome ameeleza kuwa jukumu la kuweka walinzi na kupunguza gharama ya kuchota kwa kila mradi wa maji ni jukumu la kamati za maji zilizochaguliwa na jamii na kamati hizo zinajiendesha zenyewe hivyo wao kama wanasimamia maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ili wananchi waweze kuondokana na adha hiyo na watumie maji kwa wingi kama Serikali ilivyowakusudia.
Wananchi wameishukuru Serikali kwa kuwaletea miradi hiyo ya maji ambayo kwa kiasi kikubwa imewaondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kufata huduma ya maji na kupata maji safi na salama.
Mradi wa maji Ruteme ukarabati uliofanyika ni kuweka mfumo wa sola kutoka nishati ya kutumia mafuta ya dizeli, kujenga uzio katika chanzo cha maji ambao umegharimu Tsh. 75,000,000. Mradi wa maji Kyota, ukarabati uliofanyika ni kurudisha mota na pampu zilizoharibika zilizogharimu Tsh. 30,000,000 na mradi huu unahudumia vijiji viwili vya Kagulamo na Kyota, Kata ya Kimwani.
Na mradi wa maji Kasharunga mpaka sasa ukarabati umegharimu Tsh. 189 na kazi zilizofanyika ni kulaza bomba lenye urefu wa kilomita 17, kujenga na vituo 24 vya kuchotea maji, ukarabati wa matenki mawili moja likiwa na lita za ujazo 45,000 na la pili likiwa na lita za ujazo 35,000. Kazi inayoendelea kwa sasa ni ujenzi wa tenki la kukusanyia maji lenye lita za ujazo 50,000. Mradi huu unanufaisha vijiji 4 vya Kasharunga, Nkomero, Runazi na Kiguzi vyenye wakazi zaidi ya 15,000.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa