Katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambayo yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nshambatapa kata ya Nshamba wilayani Muleba Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Emmanuel Masha amewasistiza wazazi kuhakikisha wanatoa ushirikiano kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa endapo matukio ya kiukatili yakifanyika ni vema wananchi wakatoa taarifa haraka ndani ya masaa 24 kuanzia ngazi ya familia, vijiji, kata, ustawi wa jamii na vituo vya polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wanaofanya vitendo hivyo.
"Hivi vitendo vya kiukatili vinavyotokea sio vya kuvumilia wala kuvifumbia macho inabidi tuwe na mikakati ya kuvikomesha na kuvitokomeza hivyo nawasisitiza wazazi na viongozi wote kuhakikisha vitendo vya ukatili kwa watoto vikitokea hatua kari zichukuliwe ili kutokomeza vitendo hivi" amesema Ndg. Emmanuel Masha.
Aidha, Amewomba wazazi na walezi kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anaandikishwa na kupelekwa shule na kusisitiza uongozi wa shule za msingi na Sekondari kuhakikisha wanazitumia zahanati na vituo vya afya kupima mimba kwa wanafunzi kila robo mwaka ili kupunguza mimba mashuleni.
Sambamba na hayo ametoa wito kwa jamii taasisi na mashirika kuendelea kutoa huduma za mahitaji muhimu kwa wenye virusi vya UKIMWI pamoja na watoto yatima na kutowanyanyapaa wenye virusi vya UKIMWI.
Katika risala iliyosomwa na Groly Humprey mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Nshambatapa kwa niaba ya watoto wameiomba Serikali kuhakikisha sheria ya kumlinda mtoto inazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali kwa wale watakao bainika kufanya vitendo vya ukatili kwa watoto.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika tarehe 16, juni 2022 inasema "Tuimarishe ulinzi kwa Mtoto; Tokomeza ukatili dhidi yake. Jiandae kuhesabiwa ikiwa inasisitiza kuimarishwa kwa ulinzi kwa mtoto kwa kutokomeza ukatili dhidi yake na kuwasihi wananchi wajiandae kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya watu na Makazi ya tarehe 23, Agosti 2022.
Imeandaliwa na kutolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa