Wazee ni kundi lililosahaulika kwa kuwa na hali duni ya kiuchumi. Baada ya kulibaini hilo Shirika la Wazee Nshamba, linalofanya shughuli zake wilayani Muleba liliona umuhimu wa kuanzisha mradi wa kuwasiadia wazee ujulikanao kama “Malipo ya Pensheni kwa Wazee” ambapo kwa kuanzia kila mzee mwenye umri wa miaka kuanzia 70 hulipwa pensheni ya TSH. 15,000.00 kwa mwezi . Mradi huu ulianza rasmi mwaka Novemba, 2016 kwa vijiji viwili vya Ikondokata Ikondo na Kijiji Nsisha kata Kikuku.
Kijiji kiliteua wanakamati 4 kwa ajili ya kusimamia malipo na akaunti benki. Aidha baada ya uteuzi vijiji vilifungua akaunti benki na wazee walipendekeza malipo ya pensheni yawe yanafanyika kila jumanne ya kwanza ya mwezi.
Bwana Theonist Tegarugaba wa kitongoji cha Ikondo “B”, ameeleza kuwa kabla ya kuanza kupokea pensheni hii walikuwa na hali mbaya kwa kukosa fedha za kujikimu kama kununua chakula na kwenda hospitali pale wanapoumwa lakini kwa sasa pensheni imewasaidia kupata fedha za kununua chakula, kugharamia matibabu na vifaa vya shule kwa wajukuu wanaowalea.
Aidha, alieleza kutokana na malipo haya baadhi ya wanakikundi waliona ni vema kuanzisha kikundi cha watu 12 ambapo kila mwezi mwanachama uchanga Tsh. 5,000.00 kwa ajili ya kumchangia mwanachama na hivyo anayechangiwa upewa Tsh. 70,000.00 ambayo umwezesha mwanachama kufanya jambo kubwa kama kununua mabati, sementi na kujenga nyumba. Au kuanzisha mradi wa ufugaji kuku, bata na mbuzi wa maziwa.
Naye Ndugu Almachius Tiruganya Evarist, Mwenyekiti wa Kijiji Ikondo ameshukuru sana Shirika la Wazee kubaini umaskini walionao wazee na kuona umuhimu wa kuanzisha pensheni hiyo kwa wazee. Ameeleza kuwa kama kiongozi aliyechaguliwa na wananchi anasimamia ipasavyo zoezi hili na kuhakikisha kila mzee anapata fedha yake kwa wakati.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa