Katika Kikao Maalum cha Baraza la Madiwani kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imefanikiwa kupata hati inayoridhisha.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Ndg. Toba Nguvila amesema kuwa mwenendo wa hati za ukaguzi unaonesha kuwa Halmashauri ya wilaya ya Muleba imefanikiwa kupata hati zinazoridhisha kwa kipindi cha miaka mitano hivyo amelihimiza Baraza la Madiwani pamoja na uongozi mzima wa Halmashauri kuhakikisha wanalinda mafanikio ya mwaka uliopita ili wasiweze kurudi nyuma katika ukaguzi unaoendelea.
"Ni wito wangu kwenu kuhakikisha mnaendeleza mwenendo wa utendaji kazi mzuri kwa kuepuka utendaji wa mazoea na usiozingatia taratibu kwa lengo la kuepuka hoja zisizo za lazima zinazoweza kupelekea mkapata hati ya mashaka" amesema Ndg. Toba Nguvila
Aidha, ameipongeza Halmashauri kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato ambapo kwa mwaka wa fedha 2022-2023 Halmashauri ilipanga kukusanya mapato ya ndani kiasi cha Tsh.bilioni 5.7 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha Tsh.bilioni 5.8 sawa na asilimia 101 ya lengo la mwaka.
Lakini pia amewahimiza Waheshimiwa madiwani kuhamasisha na kuhakikisha kuwa ulipaji wa kodi na tozo za Halmashauri unatekelezwa katika maeneo yao na kuhakikisha mapato yote yanayotozwa katika Halmashauri yanakatiwa sitakabadhi za mashine ya EFD.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus amesema kuwa hati safi imetokana na usimamizi madhubuti uliofanywa na Halmashauri ambapo kwa kipindi hiki Halmashauri ya wilaya ya Muleba imejaribu kuishirikisha jamii kuhakikisha kwamba kila mradi unaotekelezwa katika ngazi ya kijiji unakuwa na kamati za usimamizi na utekelezaji pamoja na usimamizi uliofanyika kwa watendaji waliopo katika ngazi za vijiji kuhakikisha wanatoa taarifa za maendeleo ya miradi.
Halmashauri ilikuwa na hoja za nyuma jumla 45 ambapo kati ya hizo hoja 19 zimetekelezwa na kufungwa, hoja 12 bado zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na na hoja 12 zimeondolewa na Mkaguzi kwa sababu mbalimbali na kubakiwa na hoja 2 ambazo hazijatekelezwa.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa