Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera imekuwa ya nne kwenye michezo ya umisseta ngazi ya taifa huku ikijinyakulia jumla ya makombe 18 ngazi ya Mkoa kwenye michezo mbalimbali iliyochezwa mwaka huu katika shule za msingi na sekondari.
Akipokea makombe hayo mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus kwenye kikao cha baraza la Madiwani robo ya nne amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 halmashauri itatenga bajeti kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi ili kukuza vipaji.
“Kupitia kikao hiki kuanzia mwaka kesho lazima tuandae bajeti ili tukuze vipaji na zaidi tutoe zawadi tuweze kuwatia moyo vijana wetu,walimu wanaowafundisha na muleba iweze kufahamika kwa kazi inazofanya”
Mhe. Magongo amewapongeza walimu wa michezo kutoka shule za msingi na sekondari kwa kushirikiana kwa pamoja kufanikisha ushindi huo ambao umeweza kuitangaza halmashauri.
“nipende kumpongeza afisa utamaduni na walimu wa michezo kwa namna wanavyotuunganisha sisi viongozi kwani kuwa mshindi wanne kitaifa sio jambo dogo hivyo niendelee kuwapongeza na niombe kila mmoja kuunga juhudi za vijana wetu”.
Kwa upande wake afisa utamaduni na michezo Wilaya ya Muleba Bw. Denis Joseph amesema wameshiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa pete, mpira wa miguu na mpira wa wavu na kuibuka kuwa mshindi wa jumla kimkoa .
Pia amesema kwa upande wa fani za ndani yaani kwanya wameshika nafasi ya kwanza kimkoa hivyo halmashauri ya Muleba ilipata nafasi ya kuwakilisha mkoa wa kagera katika mashindano ngazi ya Taifa na kuibuka mshindi wa nne.
Aidha Bw. Denis ameongeza kuwa katika mashindano ya shule za msingi wamepata makombe 7 na upande wa Sekondari makombe 11 ambapo kwenye ushindi wa jumla ngazi ya Mkoa Wilaya ya Muleba iliibuka kuwa mshindi wa kwanza kati ya Halmashauri 8.
Nao baadhi ya walimu wa michezo ambao ni Mwl. Imelda Rukatila na Mwl. Abdala Malongo wamesema kuwa ushindi walioupata umetokana na uanzishwaji wa vitalu vya michezo mashuleni pamoja na ushirikiano mkubwa waliopewa na uongozi wa Halmashauri.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa