Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Muleba, ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Mhe. Kemilembe Lwota, ameitaka Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya Mapato na kuziba mianya ya uvujaji mapato ili kuongeza makisio ya ukusanyaji wa Mapato.
Akizungumza wakati wa Baraza la kumaliza Mwaka wa fedha 2021/2022, Mhe. Kemilembe amewataka Waheshimiwa Madiwani na Wataalam kuanza kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato, huku wakiendelea kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
“Nawapongeza sana kwa ukusanyaji mapato, lakini ni wakati sasa muanze kufikiria na kubuni vyanzo vipya vya mapato. Na wakati huohuo mdhibiti upotevu wa mapato kwani Serikali isiyokusanya mapato haiwezi kuendelea,” ameeleza Mhe. Kemilembe.
Sambamba na hayo amezungumzia juu ya masuala ya kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yote ya Wilaya, huku akitoa onyo kwa watu wanaovunja amani kuwa Serikali itawachukulia sheria kali na kukemea tukio la wananchi Kijiji cha Nsambya, Kata ya Nyakabango, kuwashambulia Viongozi wa Serikali wakati wakiwa katika majukumu yao na kumjeruhi Mtendaji wa Kijiji kwa kumkata mapanga kichwani na kwenye mikono. Amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya kuwafikisha watu hao mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Ameendelea kuhamasisha maandalizi Sensa ya Watu na Makazi inayotarajia kufanyika tarehe 23.08.2022 kuwa elimu iendelee kutolewa kwa wananchi na watu wawe tayari kuhesabiwa siku hiyo kwa maendeleo ya Taifa leti.
Na mwisho amesisitiza maandalizi ya Ujio wa Mwenge wa Uhuru ambapo kwa mwaka 2022 Mkoa wa Kagera ni mwenyeji wa kilele cha mbio hizo za Mwenge Kitaifa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa