Katika ziara yake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Elias Kayandabila alipotembelea shule ya Sekondari ya Anna Tibaijuka, shule ya Sekondari Kasharunga na Shule ya Sekondari Shikizi Kasharunga kukagua mwitikio wa wanafunzi wa kadato cha kwanza kuripoti mashuleni amewasihi wanafunzi kuzingatia wanayofundishwa na walimu mashuleni.
Akizungumza alipozitembelea shule hizo Mkurugenzi Mtendaji amewasihi wanafunzi hao kuitunza miundombinu ya madarasa mapya yaliyojegwa kwa ufadhiri wa fedha za IMF ambapo katika ufadhiri huo Muleba ilipatiwa kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 208 vya sekondari na vyumba 26 vya shule za msingi shikizi.
"Fadhira pekee ambayo tunaweza kumlipa mama Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ni kufanya vizuri kwenye masomo yetu kwahiyo niwaombe sasa muweke nguvu kwenye masomo" amesema na kuwasisitiza wanafunzi Ndg. Elias Kayandabila.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji amewasihi wazazi kuisaidia Serikali kuwatambua na kuwabainisha watoto ambao kwa namna moja ama nyingine wanalazimishwa na wazazi wao kwenda kuolewa alipofika katika shule ya sekondari shikizi ya Kasharunga na kuwakuta wazazi wakiendelea na zoezi la kuwaleta shuleni hapo watoto wao.
Naye Afisa Elimu Sekondari wa wilaya ya Muleba. Mwl. Jared Muhile amewasihi wanafunzi kuvitunza vyumba vya madarasa bila kuvunja vioo kuharibu mbao za kufundishia na hata vigae vilivyotumika kujengea vyumba hivyo vya madarasa.
Kwa upande wa walimu Afisa elimu Sekondari amewasihi kuanza mala moja kuzitumia wiki sita za maelekezo kwa wanafunzi ili kuwatengenezea mwanya wa kuweza kuyaelewa watakayofundishwa na walimu.
Mwalimu Paulo Mligo Ambaye ni Mkuu wa shule ya Sekondari Anna Tibaijuka ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kutoa fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa mapya ambayo madarasa hayo yataweza kuwasaidia kuwaondolea uhaba wa vyumba vya madarasa mashuleni na kuhaidi kwamba watavitunza vyumba hivyo vya madarasa ili viweze kuwasaidia na wanafunzi wengine.
Naye mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya Sekondari Anna Tibaijuka kwa niaba ya wanafunzi wenzake ametoa shukrani na pongezi kwa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuhaidi kusoma kwa bidii ili kuweza kuzifikia ndoto zao.
Sambamba na hayo na wazazi pia na wao katika nyakati tofauti tofauti wameeeleza kuwa kupitia fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vyenye viti na meza imewaondolea changamoto ya kuchangia michango mbalimbali mashuleni hivyo kuwasaidia kuepukana na changamoto ya watoto kwenda na viti na meza mashuleni.
Shule ya Sekondari Anna Tibaijuka leo tarehe 17/1/2022 imewapokea jumla ya wanafunzi 51 ambapo idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kuripoti shuleni hapo ni wanafunzi 243 na shule ya Sekondari Kasharunga wameripoti wanafunzi 75 na idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kuripoti shuleni hapo ni wanafunzi 269.
Imeandaliwa na kutolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wilaya ya Muleba
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa