Mkuu wa wilaya ya Muleba Mh. Toba Nguvila amewasihi viongozi wa wilaya ya Muleba kusimamia ipasavyo na kuhakikisha jamii ya Muleba inaondokana na umaskini na kupata huduma bora ikiwemo elimu na afya.
Mradi wa TASAF Awamu ya pili umelenga kuendelea kuinua kaya maskini kutoka katika umaskini/hali duni na kuwawezesha walengwa kupata kipato cha kuwainua kimaisha kuweza kumudu mahitaji yao binafsi ya kila siku.
Akitoa neno kwa Wabunge, Waheshimiwa Madiwani, wakuu wa Idara na Wataalamu wanaotekeleza mradi wa TASAF awamu ya pili amewataka waheshimiwa Madiwani kusimamia na kuhakikisha walengwa watakaopendekezwa na jamii wawe ni wanufaika sahihi wenye uhitaji na sio kuchagua watu ambao sio sahihi.
"Mradi huu umekuja wakati muafaka kwa lengo la kuwaondolea umaskini wananchi wetu. Waheshimiwa Madiwani nyinyi ni watu muhimu sana katika jamii nawasihi hakikisheni mradi huu wa TASAF mna usimamia ipasavyo kama Serikali ilivyokusudia tuweze kuyafikia Malengo", alieleza Mhe. Toba Nguvila.
Aidha ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwainua wananchi na kuwaondolea umaskini hivyo kama viongozi wa wilaya ni kuhakikisha mradi huu unasimamiwa ipasavyo na kuleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Magongo Justus amewasihi Waheshimiwa Madiwani na wataaalamu kusikiliza kwa umakini na kwenda kutekeleza kama walivyoelekezwa na wawezeshaji wa TASAF makao makuu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini Mhe. Charles Mwijage amesisitiza wawezeshaji wa mradi wa TASAF awamu ya pili wasiishie tu kuwapa fedha walengwa bali wawape na elimu ya ujasiliamali ili wahitaji hao waweze kuondokana na umaskini.
Semina hii imefanyika leo tarehe 10.08.2021, katika ukumbi wa Suzana Hotel.
Imetolewa na Kitengo cha: Habari na Mawasiliano
Halmashauri ya wilaya ya Muleba
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa