Katika Baraza la Madiwani lililofanyika ndani ya Ukumbi wa Halmashauri Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amewaomba waheshimiwa madiwani kusimamia miradi yote ya serikali inayotekelezwa katika kata zao.
Akizungumza katika Balaza hilo Mkuu wa wilaya amewasihi madiwani kuhakikisha miradi yote ya Halmashauri, TARURA, TANESCO, TANROAD kuhakikisha wanaisimamia kwa sababu inawagusa wapiga kura wao.
"Niwaombe sana miradi yote simamia kila wakati tenga mda wako wa kupitia na kama kuna shida ita wataalamu wa Halmashauri waje kufanya ufafanuzi kama kukiwa na shida katika mradi wowote ita wataalamu wanaohusika na mradi huo" ameeleza Mhe Toba Nguvila.
Kwa upande wake Mhandisi wa Ujenzi Eng. Charles Solo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ameeleza kuwa mpango wa Serikali ni kuanzisha anwani za makazi ambao utakuwa ni mfumo unaotambulisha mahali ambapo mtu anaishi, mahali ilipo biashara yake, au ofisi anayofanyia kazi kwa kufuata jina la barabara na mtaa, namba ya nyumba au jengo pamoja na postikodi.
Amewaeleza Waheshimiwa madiwani kuwa dhamira ya uanzishwaji wa Anwani za makazi ni kuhakikisha utekelezaji wa anwani za makazi kabla ama ifikapo mwezi Mei, 2022 kwa kuhakikisha kila nyumba jengo lina anwani ya makazi.
Mkuu wa wilaya ameomba na kusisitiza kuhakikisha kila mtu anajipanga kwa nafasi yake kuhakikisha anashiriki vizuri katika zoezi la uanzishwaji wa anwani za makazi kuanzia uratibu utekelezaji na usimamizi mpaka kufikia mwisho wa zoezi zima.
"Ni lazma tushiriki kwa mikono yetu miwili kuhakikisha zoezi hili la anwani na makazi linafanikiwa vizuri kuliko hata Halmashauri nyingine zote" amesema Mhe. Toba Nguvila.
Sambamba na hayo amewasihi Waheshimiwa madiwani kuhakikisha wanasimamia katika kata zao ili kuondosha uvuvi haramu kwa kuwaeleza kuwa uvuvi haramu ukiendelea utadhoofisha mapato ya Halmashauri, ajira zitapotea na samaki watapungua hivyo amewaomba waheshimiwa madiwani kuhakikisha wanasimamia hilo.
Lakini pia ametoa onyo na kusisitiza kamati ya Usalama ya wilaya ya Muleba kuhakikisha wanafuatilia na kubaini mtu aliyehusika na suara la kuvujisha nyaraka ya Kiserikali ya Halmashauri kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa juu yake.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Magongo Justus amesema kuwa ameshamuagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kuanza kushughulikia suara la uvujishaji wa nyaraka ya Halmashauri ili kama ni kwa madiwani hatua za kimadili ziweze kuchukuliwa.
Imeandaliwa na Kutolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wilaya ya Muleba
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa