Mkuu wa wilaya ya Muleba Mh. Toba Nguvila amezindua rasmi soko la biashara ya samaki na dagaa katika Tarafa ya Kimwani kata Nyakabango kijiji Katembe eneo la Magarini.
Mwalo wa Katembe -Magarini, uliopo kijiji Katembe kata Nyakabango wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mialo inayotegemea sana jamii hususani ya wavuvi kwa biashara ya mazao ya samaki kutoka katika visiwa vya mazinga na Ikuza.
Akifungua soko la samaki Mkuu wa wilaya ya Muleba, Mh.Toba Nguvila amewataka wavuvi kuachana na uvuvi haramu ili kuweza kulinda raslimali za ziwa Victoria kwani kwa sasa wilaya imeweka mpango madhubuti wakulinda na kuhifadhi mazalia ya zao la samaki na kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa.
"Tumefungua Soko hili kwa sababu ya ajira kwa watu wa Muleba hasa wa eneo hili la Nyakabango kwa maana ya kwamba mama lishe watafanya biashara ya kuuza chakula kwa wageni watakao kuja kununua mazao ya samaki na vijana wetu wa Nyakabango watapata ajira ya kupakia na kushusha samaki kwa sababu kuna jengo tayari la soko la dagaa na samaki wakavu" ameeleza Mh. Toba Nguvila.
Aidha amewataka wadau wote wa uvuvi kuchangamkia fursa ya soko hilo kwani Uongozi wa wilaya umeweka utaratibi mzuri wa kuhakikisha biashara hiyo inawanufaisha watu wote watakao husika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Bw. Elias Kayandambila amesema kufunguliwa kwa soko hilo litasaidia kuwarahisishia wavuvi na wafanya biashara wamaotoka visiwani kuja kuuza mazao yao ya samaki katika Mwalo wa Katembe Magarini sambamba na kuongeza mapato kwa Halmashauri kwani zaidi ya shilingi billioni tatu za mapato yanakusanywa na Halmashauri kutokana na mapato ya uvuvi.
Pamoja na kuzindua soko hilo Mh. Toba Nguvila ameongoza zoezi la uteketezaji wa zana haramu za uvuvi zilizokamatwa maeneo mbalimbali wilayani Muleba wakati zoezi la operesheni ya kuondoa uvuvi haramu linaendelea.
Zana zilizoteketezwa ni pamoja na kokolo za kuvuta 210, timba vipande 31, Nyavu za makila (nchi 6) 51, kamba urefu wa mita 3500 na katuli 20, zana hizi haramu zinathamani ya zaidi ya shilingi milioni 197.
Kwa upande wao baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara wa samaki na dagaa wameshukuru kwa kitendo cha kufunguliwa kwa soko hilo kutokana na hapo awali walikuwa wanasafirisha kupitia kwenye soko la dagaa la wilaya jirani ya chato na walikuwa wanatozwa ghalama kubwa ya kusafirisha na tozo.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa