Akizungumza katika Kikao hicho Mkuu wa Wilaya amewaeleza waheshimiwa Madiwani kuwa wakifanya kazi za maendeleo kwa kushirikiana kama familia moja katika kutekeleza majukumu ya Serikali na kila mtu akafanya majukumu yake kama alivyokabidhiwa majukumu hayo basi watakuwa wamesaidia kukuza maendeleo ya Halmashauri.
"Tunapoingia katika utekelezaji wa majukumu ya kimaendeleo wote kwa pamoja sisi ni familia moja na tukiwa familia moja tunaweza lakini tukifanya kazi kwa kutengana hatutoweza kukidhi kiu ya wananchi ya kuwaletea maendeleo hivo ni vema tukafanya kazi kwa ushirikiano ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi na Serikali kwa ujumla" amesema Mhe. Dkt Abel Nyamahanga.
Aidha, amewahimiza waheshimiwa Madiwani kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata, Maafisa Tarafa pamoja na Wenyekiti wa Vijiji kutoa elimu kwa vijana kushiriki katika shughuli za uzalishaji kama kilimo na shughuli nyingine mbalimbali zinazoweza kuwasaidia kuinuka kiuchumi na kuweza kuwapatia mapato ambayo yataweza kuwasaidia kukidhi mahitaji yao kuliko kukaa mitaani bila kujishughulisha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus ametoa wito kwa Wataalamu kuongeza umakini zaidi katika usimamizi wa shughuli mbalimbali za utekelezaji wa miradi inayofanyika ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Akitoa Salamu za Pongezi kwa Mkuu wa Wilaya Mhe. Kalinjuma Kamili Diwani wa Kata ya Mbunda ameeleza kuwa Halmashauri tayari imeweka mkakati wa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ikiwa ni pamoja na kujenga masoko lakini ameongeza kwa kusema kuwa Halmashauri inampango wa kununua Boti itakayotumika kwa ajili ya kutatua changamoto ya usafirishaji wa wananchi wanaoishi visiwani.
Katika Taarifa iliyosomwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Dkt. Peter Nyanja amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri imefanikiwa kukusanya kiasi cha Tsh. Bilioni 7.08 ambapo jumla ya kiasi cha Tsh. Bilioni 2.1 zimepelekwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na fedha za ruzuku kutoka Serikali kuu Halmashauri ilipokea kiasi cha Tsh. Bilioni 14.2 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa