Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dr Abel Nyamahanga amewaagiza wazazi kuwapeleka watoto waliochelewa kuanza masomo ya kidato cha kwanza kuanza masomo kabla ya tarehe 10/03/2023.
Akizungumza na wazazi pamoja na wanafunzi Mkuu wa Wilaya amewasihi wazazi kutokitumia kigezo cha umasikini kama sababu ya kutowapeleka shuleni wanafunzi.
Wazazi tunatumia kigezo cha umasikini tunakwepa kutoa mahitaji kwa watoto na kuwashawishi watoto wasiende shule sasa tarehe 10 ndio mwisho wa huruma hii inapofika terehe 13 watoto wote wawe shuleni.
Aidha, amewaeleza wazazi kuwa hawawezi kukikomboa kizazi cha masikini bila kuwapeleka watoto shule hivyo ni vyema wakawapeleka watoto shule ambao wakipata elimu wataweza kuzinufaisha familia zao na kuondoa hali duni kwenye familia wanapotokea.
Lakini pia amewasihi wazazi kutowakatisha tamaa watoto wao kuikataa shule kwa kisingizio cha mazingira magumu wanayotokea ni vema wakawaelezea juu ya umuhimu wa elimu ili wawe na moyo wa kuipenda shule.
Naye Ndg. Philibert George Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyakabango ameshauri uwepo wa ufuatiliaji wa mahudhulio ya wanafunzi ambao tayari wamesharipoti mashuleni na ambao wataanza kuripoti mashuleni ili kuweza kukomesha changamoto ya wanafunzi kuhudhulia kwa mda na baadae kuacha shule.
Moses Simoni mwanafunzi aliyechelewa kuanza masomo ya kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Nyakabango ameeleza kuwa changamoto iliyomkwamisha kuanza masomo kwa wakati ni kutokana na hali ngumu ya kimaisha na kuiomba Serikali kutoa msaada kwa wenye maisha magumu ili na wao waweze kupata elimu.
Naye Vedastus Laulent ambaye pia ni mwanafunzi aliyechelewa kuanza masomo ya kidato cha kwanza ameonyesha utayari wa kuanza masomo hayo kama akisaidiwa kwa mahitaji anayopungukiwa na ameshauri kwa wanafunzi wenzake ambao na wao hawajaanza shule wasikae nyumbani waanze shule ili waweze kunufaika na elimu.
Mkuu wa Wilaya amefanya ziara hiyo katika shule ya Sekondari Nyakabango, Shule ya Sekondari Dr Ishengoma Kikoyo, Shule ya Sekondari Kimwani na Shule ya Sekondari Kyebitembe.
Imetolewa na:
kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa