Katika ziara ya kutembelea na kukagua vyanzo vya maji vilivyopo Wilayani Muleba Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dkt Abel Nyamahanga ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Muleba( MLUWASA) kupanda miti ambayo ni rafiki kwenye vyanzo vya maji ili kusaidia upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Akizungumza alipotembelea vyanzo hivyo vya maji Mkuu wa Wilaya amesema kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa kushirikiana na (MLUWASA) na wananchi wanaozunguka maeneo ya chanzo cha maji Kaigara siku ya alhamisi tarehe 13/04/2022 wataenda kupanda miti rafiki ambayo itasaidia kutunza chanzo hicho cha maji ili kiweze kudumu kwa mda mrefu.
"Nitoe wito kwa wanachi waheshimu utawala wa sheria waheshimu vyanzo vya maji wapishe maeneo yenye vyanzo vya maji ili viendelee kuwa salama katika maeneo yetu" amesema Mhe. Dkt Abel Nyamahanga.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Muleba Ndg. Evodius Mtakyamilwa amesema kuwa lengo la (MLUWASA) ni kuhakikisha wananchi wa Muleba Mjini wanapata huduma ya maji asilimia 95 na mpaka sasa asilimia 80.5 ya wananchi wanapata huduma ya maji ila changamoto inayopelekea kutofikia malengo hayo ni uvamizi wa vyanzo vya maji.
Hivyo amesema kuwa wataendelea na jitihada za kuwaelemisha wananchi kuhakikisha wanapata huduma bora za maji kwa kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu maeneo yote yanazunguka vyanzo vya maji hasa kulima pamoja na kujenga nyumba kwenye vyanzo vya maji.
Katika Ziara hiyo Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati yake ya ulinzi na Usalama ya Wilaya wametembelea na kukagua vyanzo vya maji vitatu ambavyo ni chanzo cha maji Ihako, chanzo cha maji Nyamwala na chanzo cha maji Kaigara.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa