Katika Mkutano wa baraza la Madiwani uliofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dr Abel Nyamahanga amewasisitiza Madiwani kushirikiana na viongozi pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya kubuni mbinu mpya ya kupambana na uvuvi haramu.
Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya amewasisitiza kuwa kila anayetumwa kutekeleza majukumu ya kupambana na uvuvi haramu atende kazi hiyo kwa uadirifu kama inavyostahili ili kuweza kuhakikisha suara la uvuvi haramu linaisha kabisa katika Wilaya ya Muleba.
"Asipatikane hata mtu mmoja ambaye analifumbia macho suala hili na mapambano yake lazima yawe endelevu na tuongeze kasi zaidi ya kubuni mbinu mpya maana hawa wanaojihusisha na Uvuvi haramu na wao kila siku wanabuni mbinu mpya" amesema Dr Abel Nyamahanga.
Aidha, ameshauri ukusanyaji wa makokoro na uteketezaji wake uwe wa wazi ambapo amesistiza kama makokoro yakikamatwa ijulikane na sehemu yalikochomewa.
Lakini pia ameagiza kuchukuliwa kwa juhudi za kuweza kuwabaini wanaoshirikiana na wavuvi haramu ili hatua stahiki za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao.
Sambamba na hayo ameagiza wenyekiti wa vijiji kuhakikisha wanasoma mapato na matumizi kwa wananchi ambapo amesisitiza kuwa ifikapo tarehe 30/03/2023 kila anayehusika na kusoma mapato na matumizi katika sehemu zake za vijiji awe amekwisha kusoma na taarifa zifike ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Lakini pia amesema kuwa ni vema ukawepo uanzishwaji wa benki za matofari kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika mashule ambayo hayana nyumba za walimu ili kuweza kuwasaidia walimu kutenda majukumu yao katika mazingira yaliyo bora.
Imetolewa na:
kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa