Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila katika ziara ya Ukaguzi wa Maendeleo ya ujenzi katika Kituo cha Afya Kamachumu amewahimiza Mafundi kuhakikisha wanafanya kazi bila uzembe ili kuweza kumaliza haraka upanuzi wa majengo katika kituo hicho cha afya ili kiweze kuendele kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza katika ziara hiyo amewasihi mafundi wakuu kuhakikisha kila jengo linakuwa na mafundi wasiopungua nane na wasaidizi nane pamoja na kuwahimiza Watendaji wa Kata, Afisa Tarafa na Kamati ya ujenzi kuhakikisha kila kitu kinakuwepo ili kuweza kuimarisha kazi kwa mafundi.
"Tukichelewa kuwa na mawe, kuwa na tofari kuwa na vitu vyote vinavyotokea pembezoni mwa barabara kuu tutakwama kwenye ujenzi kwahiyo mawe mchanga na tofari vyote viwe eneo husika ili mafundi wanavyoanza kujenga kusiwe na sababu yeyote inayopelekea kuchelewesha ujenzi"
Sambamba na hayo Mkuu wa wilaya ametoa pongezi kwa kuona ujenzi umeenza tangu fedha zimeingizwa kwenye akaunti terehe 13 ikiwa ni siku ya pili tangu fedha hizo kuingizwa kwenye akaunti hivyo amempongeza Mhe. Diwani na wasaidizi wake kwa kuiona kazi kwa sababu tayari wameshaweka vionwa vitakavyotumika katika ujenzi wa Kituo hicho cha afya.
Lakini pia amemuagiza Mtendaji wa Kata na Kamati ya ujenzi kuhakikisha kila siku ifikapo saa 12 wanatoa taarifa ya maeendeleo ya kazi kwa siku wamefikia hatua gani ili kuona kama kuna uzembe wowote unaoendelea achukue hatua haraka.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Mhe. Leodigard Chonde ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili upanuzi wa kituo hicho cha afya na kumhakikishia Mkuu wa wilaya kuwa akiona jambo lolote linaleta shida katika ujenzi wa Kituo cha afya atatoa taarifa na kuhaidi kusimamia usiku na mchana ujenzi huo.
Naye Mganga Mkuu wa Kituo hicho cha Afya Kamachumu Dr Lightness Charles ameleza kuwa kituo hicho kilikuwa kinapungukiwa na majengo matatu ambalo ni jengo la upasuaji jengo la mama na mama na mtoto na jengo la maabara ya kisasa.
Imetolewa na Kuandaliwa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wilaya ya Muleba
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa