Katika maadhimisho ya Siku ya Ugonjwa wa kichaa cha Mbwa Duniani yaliyofanyika Kiwilaya katika Uwanja wa Zimbihile Wilayani Muleba wananchi wameendelea kuhimizwa kuchanja mbwa wao kila baada ya mwaka ili kuwaepushia tatizo la kupata ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Akizungumza baada ya kutoa chanjo kwa baadhi ya Mbwa walioletwa na wananchi ili waweze kupatiwa chanjo hiyo Dr. Emmanuel Kaijage daktari wa mifugo wa Wilaya ya Muleba amewaelezea wananchi kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni ugonjwa ambao ni hatari sana ambao unaweza kuambukizwa kwa mbwa na huyo mbwa akamuambukiza mwanadamu kwa kumng'ata jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya mwanadamu.
"Ugonjwa wa kichaa cha mbwa hauna tiba na mnyama akishadhibitika amepata virusi hivi au binadamu akipata virusi vya kichaa cha mbwa anakuwa hawezi kupona kwahiyo ushauri tunaoutoa kwa wananchi ambao wana mbwa ni kuhakikisha mbwa wao wanapata chanjo ili mbwa akijakung'atwa na mbwa mwenye kichaa amkute huyo mbwa tayari ana kinga asiweze kupata ugonjwa" amesema Dr Kaijage.
Aidha Dr. Kaijage ameongeza kwa kusema kuwa ili kumtambua mbwa mwenye kichaa ni pale ambapo mwananchi ambaye anafuga mbwa ataona mbwa wake anatiririsha mate kutoka mdomoni pamoja kuwa na tabia ya kung'ata kitu chochote anachokiona hivyo mwananchi akiona mbwa wake anadalili hizo ni vema akachukua tahadhari.
Naye Afisa afya na Mazingira wa Wilaya ya Muleba Ndg. Johanes Francis Mutoka amesema kuwa mbwa anapokuwa amepatiwa chanjo hata aking'atwa na mbwa ambaye tayari ana virusi vya kichaa cha mbwa virusi hivo vitaweza kuangamizwa kwa sababu mbwa tayari atakuwa na kinga ya chanjo dhidi ya virusi hivyo.
Kwa upande wake Oliva Angelo mkazi wa Kata ya Muleba ameshauri kuwa ni vema wananchi wakawa wanawapeleka mbwa wao kupatiwa chanjo hata kwenye vituo vya afya ili kuweza kuwaepusha mbwa wao kupata maradhi ya kichaa cha mbwa.
Vedasto Kaigi mkazi wa Kata ya Muleba ameeleza kuwa mbwa akichanjwa inasaidia kuishi kwa amani pamoja na wananchi wengine kwani mbwa akipata ukichaa kama hajachanjwa anaweza kumjeruhi mwanadamu na kumuambukiza ugonjwa wa ukichaa jambo ambalo linaweza kuleta athari katika jamii.
Katika maadhimisho hayo jumla ya mbwa 224 na paka 31 wamepatiwa chanjo ya kichaa cha mbwa
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Kagabiro
Sanduku la Barua: 131 Muleba, Kagera
Simu: +255 (28) 222-4013
Simu:
Barua Pepe: ded@mulebadc.go.tz
Hakimilki@2017 Haki zote zimehifadhiwa